Forest yashinda Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30
Muktasari:
- Wenyeji walitangulia dakika ya 20 baada ya nahodha Morgan Gibbs-White kufunga kwa utulivu kutoka kwenye mkwaju wa penati uliotolewa kufuatia Jan Bednarek kuushika mpira.
Nottingham Forest imepata ushindi wa kihistoria, huku Viktoria Plzeň ikinusurika kupokonywa ushindi na kuilaza Roma, wakati Go Ahead Eagles ikiishangaza Aston Villa katika usiku wa kusisimua wa michuano ya UEFA Europa League Oktoba 23, 2025.
NOTTINGHAM FOREST 2-0 PORTO
Kocha mpya wa Forest, Sean Dyche, ameanza vyema baada ya timu hiyo kupata ushindi wa kwanza tangu achukue mikoba, kwa penati mbili zilizofungwa kwa ustadi na kusababisha Porto kupata kichapo cha kwanza msimu huu.
Wenyeji walitangulia dakika ya 20 baada ya nahodha Morgan Gibbs-White kufunga kwa utulivu kutoka kwenye mkwaju wa penati uliotolewa kufuatia Jan Bednarek kuushika mpira.
Wageni kutoka Ureno, ambao walishindwa kuipa kazi kubwa safu ya ulinzi ya Forest, walijikuta nyuma zaidi dakika ya 77 baada ya Igor Jesus kufunga penati ya pili kwa mpira mkali uliopigwa katikati ya goli, kufuatia Martim Fernandes kumfanyia faulo Nicolò Savona ndani ya boksi.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Forest katika michuano ya Ulaya ikiwa imepita takribani miaka 30 baada ya 1995 kuichapa Lyon bao 1-0.
ROMA 1-2 VIKTORIA PLZEŇ
Roma walipokea kipigo cha pili mfululizo nyumbani kwenye Europa League baada ya Viktoria Plzeň kufunga mabao mawili kwa dakika mbili pekee na kuwashangaza wenyeji.
Wageni walichukua udhibiti wa mchezo kipindi cha kwanza kupitia mabao ya Prince Kwabena Adu na Cheick Souaré.
Paulo Dybala alirejesha tumaini kwa Roma kwa kufunga penati likiwa ni goli lake la 200 katika maisha yake ya soka, lakini Plzeň walijilinda vyema hadi mwisho, kumpa kocha mpya Martin Hyský mwanzo mzuri katika kampeni yake ya Ulaya.
GO AHEAD EAGLES 2-1 ASTON VILLA
Nahodha Mats Deijl alifunga bao la ushindi lililowapa Go Ahead Eagles ushindi wa pili mfululizo kwa kutoka nyuma.
Mshambuliaji wa Villa, Evann Guessand alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 4, lakini baadaye akanyimwa nafasi ya pili ya kufunga na kipa Jari De Busser katika uso kwa uso.
Mathis Suray alisawazisha dakika ya 42 kwa kombora la kiufundi ndani ya eneo la hatari goli lao la kwanza kabisa nyumbani katika hatua ya makundi kabla ya Deijl kufunga kwa utulivu dakika ya 61.
Emiliano Buendía alipoteza nafasi ya kusawazisha baada ya kupiga juu ya lango penati dakika 11 kabla ya mwisho, na Villa wakabaki na pointi zao sita.
FENERBAHÇE 1-0 STUTTGART
Mchezaji wa wa Uturuki alihakikisha Fenerbahçe wanapata ushindi wa pili mfululizo nyumbani katika hatua ya makundi baada ya kufunga kwa penati kwa ustadi, akimdanganya kipa Alexander Nübel wa Stuttgart, goli lake la tatu kwenye mashindano haya na kumfanya kuwa mfungaji kinara kwa sasa.
Mchezo huo haukuwa na nafasi nyingi wazi, huku mshambuliaji Deniz Undav akikosa nafasi bora zaidi kwa wageni dakika ya 82 alipoupiga mpira pembeni mwa goli, na kuwaacha Stuttgart wakiwa na pointi tatu pekee baada ya mechi tatu.
MATOKEO
Salzburg 2-3 Ferencváros
Fenerbahçe 1-0 Stuttgart
FCSB 1-2 Bologna
Go Ahead Eagles 2-1 Aston Villa
Genk 0-0 Real Betis
Lyon 2-0 Basel
Braga 2-0 Crvena Zvezda
Brann 3-0 Rangers
Roma 1-2 Viktoria Plzeň
Young Boys 3-2 Ludogorets
Celtic 2-1 Sturm Graz
Lille 3-4 PAOK
Maccabi Tel-Aviv 0-3 Midtjylland
Malmö 1-1 GNK Dinamo
Nottingham Forest 2-0 Porto
Celta 2-1 Nice
Freiburg 2-0 Utrecht
Feyenoord 3-1 Panathinaikos