Floyd Mayweather Jr atajwa kuwa bondia bora wa muda wote, Mwakinyo asogea mdogo mdogo

Wednesday September 15 2021
may pic

Licha ya kutokuwa hai kwenye ndondi za kulipwa, bondia Floyd Mayweather Jr ametajwa kuwa bondia namba moja duniani kwa ubora.

Mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (boxrec) umemtaja bondia huyo Mmarekani kuwa namba moja kwenye orodha ya mabondia wote wa dunia katika kila uzani 'pound for pound' huku Mtanzania, Hassan Mwakinyo akiambulia nafasi ya 178.

Mayweather Jr ambaye mara ya mwisho alipanda ulingoni Juni mwaka huu ameendelea kuwa namba moja duniani katika orodha ya mabondia hai na waliostaafu akiwa na pointi 3568 kwenye mapambano 50 aliyocheza na kushinda yote.

Hasimu wake Manny Pacquiao anayepigania pia uzani wa welter, licha ya kutoonekana ulingoni kwa muda mrefu amekamata nafasi ya nne katika orodha ya mabondia bora wa dunia kwenye kila uzani.

Hata hivyo, bondia namba moja kwenye pound for pound ya dunia kwa mabondia walio hai, Saul Alvarez raia wa Mexico ametajwa kwenye nafasi ya 10 katika orodha ya mabondia bora wa muda wote.

Alvarez mwenye pointi 1159 anayepigania uzani wa super middle ameachwa na Mayweather Jr kwa pointi 2409.

Advertisement

Wengine walioingia kwenye orodha ya mabondia bora wa muda wote kwa mujibu wa Boxrec ni Ezzard Charles bondia wa uzani wa light heavy aliyekamata nafasi ya pili na Bernard Hopkins amehitimisha tatu bora.

Wengine ni Pacquiao, Andre Ward, Joe Calzaghe, Lennox Lewis, Archie Moore na nguli wa zamani wa uzani wa juu, Wladimir Klitschko aliyestaafu baada ya kuchapwa kwa Technical Knock Out (TKO) na Anthony Joshua bondia namba moja kwenye uzani wa juu na namba nne kwenye pound for pound ya mabondia walio hai ingawa kwenye orodha ya mabondia bora wa muda wote ameangushwa.

Katika orodha hiyo, kwa mabondia walio hai, Mwakinyo bondia namba moja nchini ametajwa kuwa wa 178 kati ya 18097 huku Ibrahim Class akiwa ni Mtanzania aliyefuatia kwa kufanya vizuri akiwa nafasi ya 588.

Advertisement