Fenerbahce yatua kwa Ederson, Donnarumma kicheko
Muktasari:
- Fenerbahce imeanza mazungumzo ya kumsajili Ederson, baada ya wapinzani wao wa jadi nchini Uturuki, Galatasaray, kushindwa kufanikisha kumsajili licha ya kufanya mazungumzo na wawakilishi wake pamoja na Man City wiki kadhaa zilizopita.
ISTANBUL, UTURUKI: KWA mujibu wa ripoti, klabu ya Fenerbahce ya Uturuki sasa ipo katika mazungumzo ya kumsajili kipa wa Manchester City, Ederson hali inayoliweka hai dili la Gianluigi Donnarumma kutua jijini Manchester katika dirisha hili baada ya hapo awali mambo kuonekana kuwa magumu kutokana na kujiondoa kwa Galatasaray katika mpango wa kumsajili Ederson.
Fenerbahce imeanza mazungumzo ya kumsajili Ederson, baada ya wapinzani wao wa jadi nchini Uturuki, Galatasaray, kushindwa kufanikisha kumsajili licha ya kufanya mazungumzo na wawakilishi wake pamoja na Man City wiki kadhaa zilizopita.
Inaelezwa changamoto kubwa iliyosababisha Galatasaray kuachana na mpango wa kumsajili kipa huyo ilikuwa ni ada ya Euro 10 milioni iliyohitajika na Man City.
Galatasaray ilikuwa tayari kulipa kiasi kisichozidi Euro 5 milioni kwa ajili ya kipa huyo wa kimataifa wa Brazil, dau ambalo Man City iligoma.
Ederson ameichezea Man City michezo 372, lakini msimu huu wa 2025/26 ameanza benchi akiwa namba mbili nyuma ya kipa mpya James Trafford, aliyesajiliwa katika dirisha hili la majira ya kiangazi hata baada ya kupona ugonjwa uliomsababisha kukosa mechi ya ufunguzi.
Ikiwa Fenerbahce itakubali kutoa ada ya uhamisho inayohitajika, Man City inaweza kufanikisha mchakato wa kumsajili Donnarumma, ambaye naye anataka kuondoka PSG baada ya kocha Luis Enrique kuweka wazi kuwa hamhitaji.
Ederson yuko katika miezi 12 ya mwisho ya mkataba wake na tayari kulikuwa na dalili kwamba ataondoka katika dirisha hili, hasa baada ya kuhusishwa na baadhi ya timu za Saudi Arabia mwaka jana.
Licha ya kwamba dirisha la usajili barani Ulaya linafungwa leo saa sita usiku, ili Man City kumwachia fundi huyu na kufanikisha mchakato wa kumsajili Donnarumma itatakiwa kufikia makubaliano na Fenerbahce kabla ya dirisha la usajili kufungwa leo kwani haitaki kumwachia Ederson kabla ya kuwa na uhakika wa kumpata Donnarumma.