Fainali za Afrika 2025 zamtisha Amorim
Muktasari:
- Nyota hao watatu, Bryan Mbeumo, Noussair Mazraoui na Amad Diallo watakuwa na vikosi vya nchi zao, Cameroon, Morocco na Ivory Coast mtawalia katika fainali za Afcon na hivyo kumpasua kichwa Amorim kwa kuona timu itapitia changamoto kubwa.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim anafikiria kuomba kucheleweshwa kwa safari ya mastaa wake watakaoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), kutokana na ratiba ya mechi zijazo.
Nyota hao watatu, Bryan Mbeumo, Noussair Mazraoui na Amad Diallo watakuwa na vikosi vya nchi zao, Cameroon, Morocco na Ivory Coast mtawalia katika fainali za Afcon na hivyo kumpasua kichwa Amorim kwa kuona timu itapitia changamoto kubwa.
Fainali hizo zitakazofanyika Morocco 2026, zitaanza 21 hadi Januari 18 na baadhi ya nyota wa Ligi Kuu England watalazimika kusafiri kuzitumikia timu zao za taifa na kusababisha vikosi vingi vya klabu za Ligi Kuu England kukuna kichwa namna ya kuziba mapengo yao katika kipindi hicho ligi ikiwa inaendelea.
Kutokana na hilo, Man United inataka kuzungumza na mashirikisho ya nchi wanazotoka nyota wao, kuchelewesha safari ya kwenda Morocco ili wawatumie katika mechi za kabla ya kuanza fainali hizo.
Man united ambayo imekuwa na kiwango kizuri tangu kuanza msimu huu, Kocha Amorim anajivunia nyota wake ambao wamekuwa na mfululizo wa matokeo mazuri na kupanda viwango na jana usiku ilikuwa na mechi dhidi ya Everton ikisaka pointi tatu kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Pia kutokana na changamoto hiyo ya kuondoka kwa nyota huyo, Amorim ameomba nyota wake wengine wanaotaka kuondoka dirisha la usajili la Januari wakiwamo Joshua Zirkzee na Kobbie Mainoo, wasiondoke, huku akimwonya kiungo Mreno aliyenunuliwa kwa Pauni 50.75 milioni, Manuel Ugarte kuhusu kiwango chake mazoezini.
“Wachezaji wengi wazuri wanakuja hapa na wakati mwingine wanapata shida,” Amorim alisema. “Kwa sasa (Ugarte) anapata shida.
“Kazi yangu ni kumsaidia ajihisi kama mchezaji, kama alivyokuwa Sporting, kwa mfano.
“Lakini ulimwengu ni tofauti na anahitaji kuzoea na kuboresha kiwango hasa mazoezini.”
Amorim pia ameanza kuangalia nyota watakaoziba nafasi zao akiwamo kinda Jack Fletcher, 18, aliyekaa benchi katika mchezo dhidi ya Tottenham wiki mbili zilizopita, pamoja na Shea Lacey aliyefanya mazoezi na kikosi cha kwanza Ijumaa iliyopita.
“Lazima tutapata changamoto na lazima tujiandae kwa hilo,” alisema Amorim na kuongeza,
“Itakuwa ngumu ikifika kipindi hicho, lakini itabidi tuzoee. Tulipitia vikwazo vingi mwaka jana na tulibadilika.”