Fabregas akitoka, Ten Hag anaingia Como

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Florian Plettenberg ambaye ni mwandishi wa habari kutoka Ujerumani, Leverkusen iko kwenye mazungumzo na Como kuhusu uwezekano wa kuipata huduma ya Fabregas kama mrithi wa Xabi Alonso na bado hadi sasa hawajafikia mwafaka.
LEVERKUSEN, UJERUMANI: KOCHA wa zamani wa Manchester United, Erik ten Hag anaweza kuwa kocha mpya wa Bayer Leverkusen ikiwa Cesc Fabregas ataamua kuendelea kusalia Como.
Kwa mujibu wa Florian Plettenberg ambaye ni mwandishi wa habari kutoka Ujerumani, Leverkusen iko kwenye mazungumzo na Como kuhusu uwezekano wa kuipata huduma ya Fabregas kama mrithi wa Xabi Alonso na bado hadi sasa hawajafikia mwafaka.
Como inadaiwa haiko tayari kumruhusu kiungo huyo wa zamani wa Arsenal kuondoka kwa urahisi kwani bado wanahitaji aendelee kukinoa kikosi chao.
Leverkusen imepanga kupambana hadi mwisho ili kuhakikisha inampata staa huyu lakini ikishindikana imepanga kuhamia kwa chaguo lao la pili ambalo ni Ten Hag.
Kocha huyo raia wa Uholanzi hajapata kazi tangu alipoondoka Man United Oktoba mwaka jana, baada ya timu hiyo kushinda mechi tatu pekee kati ya tisa za mwanzo wa msimu.
Hata hivyo, licha ya yeye kuondoka hali ya timu hiyo imezidi kudorora, jambo linaloonyesha tatizo kubwa halikuwa yeye.
Leverkusen ambayo ilishinda taji la Bundesliga chini ya Xabi Alonso imesisitiza hadi sasa hakuna kocha aliyekataa kujiunga nao na hakuna kocha yoyote waliyemchagua.
"Hakuna kocha aliyekataa kuwa nasi hadi sasa. Ninaamini tutamaliza hili ndani ya mwezi huu na tuko katika hatua za mwisho. Hili litakamilika Mei hii kwa hakika," alisema Simon Rolfes ambaye ni mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo.