Fabregas aduwaza, AC Milan, Juve chali Ulaya
Muktasari:
- Ushindi wa Como, pamoja na kipigo cha mabao 2-1 ilichopata AC Milan kutoka kwa Cagliari, ulihakikisha Como wanamaliza nafasi ya nne, huku kichapo hicho kikithibitisha kushuka daraja kwa Cremonese.
ROMA, ITALIA: Miujiza ya kocha Cesc Fabregas imeonekana baada ya kuiongoza Como kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia yake kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Cremonese katika mchezo wa mwisho wa msimu wa Serie A.
Ushindi wa Como, pamoja na kipigo cha mabao 2-1 ilichopata AC Milan kutoka kwa Cagliari, ulihakikisha Como wanamaliza nafasi ya nne, huku kichapo hicho kikithibitisha kushuka daraja kwa Cremonese.
“Ni moja ya mafanikio yangu makubwa kutokana na namna tulivyolifanya na watu tuliokuwa nao, kwa sababu tumefanya hili na wachezaji vijana, karibu wote wana chini ya miaka 23. Hii ni ya kushangaza,” amesema Fabregas, mwenye miaka 39, ambaye aliwahi kuchezea Arsenal, Chelsea na FC Barcelona.
Mabao ya Jesus Rodriguez na Tasos Douvikas yaliipa Como uongozi mzuri mapema kabla ya Jamie Vardy kuangushwa ndani ya eneo la hatari, na Federico Bonazzoli kufunga penalti iliyowapa wenyeji matumaini.
Kikosi cha Fabregas kilipata penalti yenye utata dakika 20 kabla ya mwisho, jambo lililosababisha kadi nyekundu tatu kwa wachezaji wa Cremonese.
Kiungo Alberto Grassi alitolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kutokana na malalamiko yake, huku Milan Đurić na David Okereke, waliokuwa benchi, pia wakitolewa kutokana na vurugu zilizotokea.
Lucas Da Cunha alifunga bao la nne mwishoni na kuipa Como ushindi wa kihistoria pamoja na tiketi ya Ulaya kwa timu iliyorudi Serie A misimu miwili tu iliyopita.
Kabla ya mchezo huo, Como walijua walihitaji kushinda huku wakisubiri aidha Milan au AS Roma kupoteza pointi ili wafuzu.
Roma waliibuka na ushindi dhidi ya Hellas Verona na kumaliza nafasi ya tatu, lakini kipigo cha Milan dhidi ya Cagliari kiliiwezesha Como kuipiku timu hiyo yenye mataji saba ya Ligi ya Mabingwa.