Vigogo Italia wakabana kufuzu Ligi ya Mabingwa
Muktasari:
- Tayari Inter Milan wametwaa ubingwa ikiwa na pointi 86, huku Napoli ikiwa ya pili na pointi 73, wakijihakikisha nafasi yao ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Roma, Italia: Pazia la Ligi Kuu Italia ‘Serie A’ 2025/26 litafungwa kesho macho yote yapo kwa timu nne zinazowania nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Tayari Inter Milan wametwaa ubingwa ikiwa na pointi 86, huku Napoli ikiwa ya pili na pointi 73, wakijihakikisha nafasi yao ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Macho yote yamebaki kwa timu nne zinapigana vikumbo kuwania nafasi mbili zilizobaki ambao ni AC Milan iliyonafasi ya tatu na (pointi 70), AS Roma ya nne (pointi 70), wakati Como ipo nafasi ya tano (pointi 68), huku Juventus wakiwa nafasi ya sita(pointi 68).
Katika mbio hizo za kuwania nafasi hizo mbili AC Milan na Roma wako katika mazingira mazuri zaidi iwapo watashinda mechi zao za mwisho.
Mabingwa mara saba wa Ligi ya Mabingwa, Milan wenyewe watakuwa nyumbani kuwakaribisha Cagliari, wakati AS Roma watakuwa ugenini dhidi ya Hellas Verona. Iwapo timu hizo mbili zitashinda, zitafuzu moja kwa moja kwa Ligi ya Mabingwa bila kujali matokeo ya wengine.
Hatahivyo; bado Como na Juventus wana matumaini kwa kutegemea wawili wa juu watapoteza mechi zao au kutoa sare na wenyewe kushinda.
Kocha Cesc Fabregas na kikosi chake cha Como watasafiri kucheza dhidi ya Cremonese, huku Juventus wakikabiliana na Torino katika derby kali ya Turin. Lazima washinde mechi zao huku wakiomba angalau mmoja kati ya AC Milan au Roma apoteze pointi katika mechi zao za mwisho.
Siku ya mwisho ina kila kitu: presha, hesabu za pointi na ndoto za Ligi ya Mabingwa. Timu mbili zitafurahia usiku wa kihistoria, huku nyingine mbili zikibaki na majuto.