Everton yapewa masharti magumu kusajili Grealish
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, Everton tayari ilishawasiliana na Man City kuanzisha mazungumzo juu ya uwezekano wa kumsajili Grealish kwa mkopo wa msimu mmoja na kusisitiza ipo tayari kulipa sehemu ya mshahara wake ambao ni Pauni 300,000 kwa wiki.
MANCHESTER, ENGLAND: INAELEZWA Everton ipo tayari kumsajili mshambuliaji wa Manchester City, Jack Grealish lakini inakumbana na masharti magumu ambayo huenda yakasababisha iachane na mpango huo.
Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, Everton tayari ilishawasiliana na Man City kuanzisha mazungumzo juu ya uwezekano wa kumsajili Grealish kwa mkopo wa msimu mmoja na kusisitiza ipo tayari kulipa sehemu ya mshahara wake ambao ni Pauni 300,000 kwa wiki.
Hata hivyo, kwa mujibu wa tovuti ya talkSPORT, Manchester City hawatakubali ofa yoyote ya mkopo isipokuwa klabu inayomtaka ikubali kulipa mshahara wote wa Grealish kwa msimu ujao.
Grealish, ambaye bado ana miaka miwili katika mkataba wake wa sasa, alipoteza nafasi ya kuaminiwa chini ya Pep Guardiola msimu uliopita na sasa amekubali anakaribia kuondoka Etihad.
Mbali na Everton, Tottenham Hotspur na Napoli pia zinamfuatilia kwa karibu na inadaiwa mchezaji huyo anataka kuendelea kucheza England licha ya timu kibao za nje kuhitaji huduma yake.
Hivi karibuni Grealish alikataa ofa ya kujiunga na Fenerbahce ya Uturuki inayofundishwa na Jose Mourinho. Timu hii inadaiwa ilikuwa tayari kulipa mshahara wake wote kwa msimu mmoja na kumsajili kwa mkopo ambao una kipengele cha kumnunua jumla mwisho wa msimu.
Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 29 hakushiriki katika mechi ya kwanza ya maandalizi ya msimu mpya ya Man City dhidi ya Preston, iliyochezwa bila ya mashabiki mapema wiki hii.
Vilevile hatosafiri na kikosi cha Man City kwenda Italia, ambako klabu hiyo itacheza dhidi ya Palermo, Jumamosi ua wiki hii katika mechi nyingine ya maandalizi.
Mbali ya sharti la kutaka mshahara wake wote kulipwa, Man City pia inataka timu inayomhitaji Grealish kwa mkopo kuweka ofa ya kumnunua jumla mwisho wa msimu.