Euro 2024 ukizubaa unapigwa
Muktasari:
- Mechi hiyo itazamiwa kuwa na bato nyingi za uwanjani, ambazo zitafanya mashabiki kupata burudani ya kutosha kabisa.
MUNICH, UJERUMANI: BALAA hilo. Nusu fainali ya kwanza ya EURO 2024 itapigwa usiku wa leo Jumanne, wakati Hispania itakapoonyeshana kazi na Ufaransa katika kipute kitakachopigwa huko Munich.
Mechi hiyo itazamiwa kuwa na bato nyingi za uwanjani, ambazo zitafanya mashabiki kupata burudani ya kutosha kabisa.
Ukiweka kando kipute hicho cha leo, kesho Jumatano uhondo utaendelea, ambapo Uholanzi itamaliza ubishi na England.
Kwenye kipute cha Hispania na Ufaransa kutakuwa na bato la vijana dhidi ya wachezaji wenye uzoefu.
Hispania haitakuwa na huduma ya wazoefu Dani Carvajal na Robin Le Normand kutokana na kukabiliwa na adhabu za kadi, hivyo kocha Luis de la Fuente atalazimika kumpanga mzoefu mwingine Jesus Navas kwenye beki ya kulia. Na mkongwe huyo, atakuwa kwenye balaa zito la kukabiliana na vijana ambao kama hatakuwa Kylian Mbappe basi atakuwa Ousmane Dembele au Bradley Barcola. Shughuli anayo.
Kwa mchezaji yeyote atakayekuwa na majukumu ya kumkaba Mbappe na Dembele anahitaji kuwa fiti kwelikweli kutokana na vijana hao kuwa na kasi kubwa. Lakini, Navas ni mchezaji mwenye kasi pia, kilichopo ni kusubiri kuona kama umri haujaanza kumtupa mkono.
Lakini, balaa litakalowahusu Ufaransa kwenye mechi hiyo ni namna ya kukabiliana na mawinga wa Hispania. Kama kuna eneo ambalo bila ya shaka kocha wa Les Bleus, Didier Deschamps atakuwa kweye shaka kubwa ya kukosa usingizi ni juu ya kuwadhibiti makinda wawili, tishio kwenye wingi, Lamine Yamal na Nico Williams.
Jules Kounde bila shaka atakuwa kwenye kazi nzito ya kumkabili Williams, huku upande wa pili utakuwa na kasheshe la Yamal na Theo Hernandez, kufanya mechi hiyo kuwa na mvuto mkubwa wa kuitazama.
Kwenye sehemu ya kati ya uwanja kutakuwa na vita nyingine ya Rodri na N’Golo Kante. Viungo hao wote ni wenye uzoefu mkubwa, hivyo eneo hilo litakuwa na mchango mkubwa katika kuamua mchezo huo matata kabisa.
Kasheshe la mchezo wa kesho baina ya England na Uholanzi, inatajwa ni vita ya Ligi Kuu England. Hilo linatokana na mastaa kadhaa muhimu kwenye kikosi cha Orenji baadhi kuendelea kucheza kwenye Ligi Kuu England kama Virgil van Dijk na Cody Gakpo, huku wengine wakiwahi kupita kwenye ligi hiyo, kama vile Memphis Depay, hivyo wanakwenda kukutana na wachezaji ambao wamekuwa wakikutana mara kwa mara.
Kipute hicho ni cha kujuana, hivyo ni mechi ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa kuona ni timu gani itatinga fainali. England ilitinga fainali katika Euro 2020 na kujikuta ikichapwa kwa mikwaju ya penalti na Italia. Safari hii mambo yatakuwaje?
Wakongwe wa soka nchini, Sekilojo Chambua, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, Joseph Kaniki ‘Golota’ na Athumani Idd ‘Chuji’ wametabiri ushindani mkubwa wa timu nne zilizoingia nusu fainali ya mashindano ya Mataifa ya Ulaya kuwa zina uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo. Wakongwe hao walisema hayo wakati wa uzinduzi wa msimu mpya wa Mbungi Bampa2Bampa.
Malima alisema kuwa timu zote nne, Hispania, Ufaransa, England na Uholanzi zina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.