Esperance yazinduka, yavuna mabilioni, Bayern ikitinga 16 Bora CWC

Muktasari:
- Esperance ilipata ushindi huo usiku wa kuamkia leo Jumamosi katika mechi ya Kundi D, huku wenyeji wakipoteza penalti sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo uliopigwa Nashville.
WAWAKILISHI wa Afrika katika fainali za Kombe Dunia la Klabu (CWC) 2025, Esperance ya Tunisia imezinduka kwa kupata ushindi dhidi ya Los Angeles ya Marekani na kuvuna mkwanja wa maana unaotolewa kwa kila ushindi hatua ya makundi.
Esperance ilipata ushindi huo usiku wa kuamkia leo Jumamosi katika mechi ya Kundi D, huku wenyeji wakipoteza penalti sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo uliopigwa Nashville.
Bao lililofufua tumaini kwa Esperance la kutinga hatua ya 16 Bora iwapo itapata ushindi mbele ya Chelsea Jumatano ijayo liliwekwa kimiani dakika ya 71 kupitia Youcef Belaili.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa Esperance baada ya awali kuanza michuano kwa kipigo cha 2-0 kutoka kwa vinara wa kundi hilo, Flamengo ya Brazil iliyofuzu 16 kwa kukusanya pointi 6 hadi sasa baada ya kuizima Chelsea kwa mabao 2-1 jana usiku.
Ushindi huo umeifanya Esperance kuvuna Dola 2Milioni sawa na Sh 5.2 Bilioni zinazotolewa kwa kila timu inayoshinda hatua ya makundi.
Hata hivyo, Esperance watamshukuru Denis Bouanga wa Los Angeles aliyekosa penalti dakika ya 90+11.
Hii inakuwa timu ya pili kati ya nne za Afrika kupata ushindi katika michuano hiyo baada ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyoifunga Ulsain HD ya Korea Kusini kwa bao 1-0 na usiku wa leo itashuka tena uwanjani kuvaana na Borussia Dortmund ya Ujerumani, mechi ya Kundi F.
Wawakilishi wengine wa Afrika Al Ahly ya Misri iliyopo Kundi A ilianza na sare kabla ya kupoteza mechi ya pili, wakati Wydad AC ya Morocco ilipoteza 2-0 mbele ya Man City ya England katika Kundi D.
Hadi sasa Bayern Munich, Batafogo na Flamengo zimefuzu 16 Bora kwa kila moja kukusanya pointi sita katika makundi yao.
Mbali na mechi ya Dortmund na Mamelodi inayopigwa saa 1 usiku, leo pia kutakuwa na mechi nyingine saa 4 usiku kati ya Inter Milan na Urawa Reds.
Michuano hiyo inashirikisha timu 32 zikizopangwa nne nne katika makundi manane na itafikia tamati Julai 13 na Bingwa atavuna Dola 40 Milioni sawa na Sh105 Bilioni.