ERIKSEN... Filamu inayoendelea kuishi

MANCHESTER, ENGLAND. ILE comeback inaendelea. Hii inaweza kutengeneza stori nzuri ya filamu huko Hollywood. Ni miezi 15 tu iliyopita, Christian Eriksen alikuwa anapambania maisha baada ya kupata mshtuko wa moyo na kuanguka uwanjani kwenye mechi ya Euro 2020. Fundi huyo wa mpira kutoka Denmark, mwenye umri wa miaka 30, alijikuta mkataba wake ukisitishwa Inter Milan kwa sababu tu, mshtuko wa moyo aliyopata ulisababishwa awekewe kifaa maalumu kwenye moyo kitu ambacho kwa sheria za soka la Italia, mchezaji aliyewekewa kifaa cha aina hiyo, haruhusiwi kucheza.

Brentford wakampa nafasi ya kurudi uwanjani baada ya kumsainisha mkataba wa miezi sita Januari mwaka huu, akacheza soka la kiwango bora kabisa na kuwavutia wengi.

Manchester United wakavutika na kumpa ofa ya dili tamu na msimu huu alikuwa staa wa mchezo kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Arsenal uwanjani Old Trafford.

Na sasa anaonekana kuwa yupo tayari kwa ajili ya Kombe la Dunia - akionyesha kiwango moto katika kwenye mechi dhidi ya Ufaransa na kuvunja rekodi kwenye michuano ya UEFA Nations League.


Alikufa kwa dakika tano

Kwa namna Eriksen anavyotamba uwanjani kwa sasa ni kama muujiza kutokana na lile lililomtokea akiwa uwanjani Parken Stadium, Juni 12, 2021. Akiwa hana mpira, Eriksen alianguka na kwa haraka mchezo ukasimamishwa. Umma wa mashabiki wa soka duniani walishuhudia kupitia runinga zao namna kiungo huyo alivyokuwa akipambana na uhai kufuatia kupatwa na shambulio la moyo.

Nahodha wa Denmark, Simon Kjaer alikimbia kwa haraka kutoa huduma ya kwanza, kabla ya kuwapanga wachezaji wenzake kutengeneza mduara kuweka faragha ya mchezaji mwenzao wakati alipokuwa akipatiwa tiba. Akapewa tiba ya kushtuliwa moyo na bahati nzuri, moyo ukaamka na kuanza kufanya kazi tena.

“Nilikuwa nimekwenda kwa dakika tano nzima,” alisema Eriksen alipozungumza na BBC.


Ameamka, yupo tayari kwa mapambano

Siku tatu baadaye baada ya kupata tatizo hilo uwnajani, Eriksen alituma picha yake kwenye mitandao ya kijamii akionyesha dole gumba kwamba yupo fiti wakati akiwa amelala kwenye kitanda kimoja katika hospitali ya Copenhagen na kuwaambia mashabiki wa soka kwamba yupo vizuri akiendelea na uchunguzi. Eriksen alisema hatakataa tamaa na kuahidi huo usingekuwa mwisho wake.

Kutengeneza uhakika wa kurudi tena uwanjani na kucheza mpira, Eriksen aliendelea kuwekewa kifaa maalumu kwenye moyo wake Implantable Cardioverter Defibrillator, kwa ajili ya kuufanya moyo kuanza upya kufanya kazi baada ya kupata mshtuko. Ni kifaa chenye ukubwa wa nusu laini ya simu ambacho kina waya zinawekwa kwenye moyo. Kwa soka la Italia, mchezaji aliyewekewa kifaa kama hicho haruhusiwi kucheza, hivyo Eriksen hataonekana tena kwenye soka la nchi hiyo. Akabaki njiapanda.


Mkataba wake utasitishwa

Kutokana na sheria hiyo, Inter Milan hawakuwa na chaguo jingine zaidi ya kusitisha mkataba wa Eriksen. Walifikia makubaliano ya kuvunja mkataba huku Inter Milan wakiomba radhi kutokana na lile linalofanyika. “Klabu na familia nzima ya Nerazzurri inamtakia Christian kila la heri katika maisha yake ya baadaye,” ilisomeka yake.

“Ingawa Inter na Christian wanaachana kwa sasa, uhusiano wetu hautavunjika. Nyakati nzuri, mabao, ushindi na kushangilia ubingwa wa Scudetto nje ya uwanja wa San Siro na mashabiki wetu vitabaki kwenye historia ya Nerazzurri.”

Hayo yakamfanya Eriksen aanze kujipanga upya kwa ajili ya maisha yake ya baadaye.


Akarudi Ligi Kuu England

Kwenye dirisha la Januari, Eriksen alirudi kukipiga kwenye Ligi Kuu England safari hii akienda kujiunga na Brentford.

Kocha Thomas Frank, ambaye alifanya kazi ya Eriksen wakati anachezea timu za vijana huko Denmark, alimvuta kwenye kikosi chake cha Brentford na kumpa nafasi ya kufurahia tena kucheza soka.

Baada ya siku 27, Brentford ilimtangaza Eriksen kuwa mchezaji wao, wakimpa dili la miezi sita tu kutamba tena uwanjani. Alipoingia uwanjani kuchukua nafasi ya Mathias Jensen kwenye mechi ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Newcastle United, Eriksen alipewa heshima ya kushangiliwa na mashabiki wote wakiwa wamesimama uwanjani wakati anaingia.

Wiki mbili baadaye, Eriksen aliandika rekodi yake ya kwanza Brentford alipotoa asisti kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burnley. Kisha Aprili, alikuwa staa wa mchezo Brentford ilipoiduwaza Chelsea kwa kuwachapa mabao 4-1 Stamford Bridge - ambapo alifunga bao lake la kwanza baada ya kurejea kwenye soka tena. Kitu kinachovutia, Erikseni rekodi zake tangu alipoanza kuichezea Brentford wakati msimu unakwisha ni Kevin De Bruyne na Martin Odegaard peke yao ndiyo walikuwa wametengeneza nafasi nyingi Ligi Kuu England kumzidi.


Stori inaendelea

Baada ya kurejea kibabe kabisa kwenye Ligi Kuu England, Eriksen akaanza kuripotiwa kusakwa na klabu yake ya zamani ya Tottenham Hotspur, wakati huo Brentford wakiamini kwamba atabaki kwenye kikosi chao huko London Magharibi.

Lakini, hapo ikatokea nafasi ya kwenda kuwa chini ya kocha Erik ten Hag huko Old Trafford, hivyo Eriksen alikubali kujiunga na Manchester United kwa uhamisho wa bure. Mwanzoni, maisha yalitikiswa kidogo. Kichapo cha nyumbani Old Trafford kutoka kwa Brighton kikafuatiwa na kipigo kizito cha mabao 4-0 kutoka kwa timu yake ya zamani ya Brentford. Mbaya zaidi, Eriksen alihusika kwenye moja ya mabao hayo.

Lakini, haikuchukua muda mrefu alirejea maisha Man United kuwa salama baada ya kupata ushindi dhidi ya Liverpool, Southampton na Leicester. Eriksen akaanza kuonyesha ubora miguuni. Akawafanya jambo Arsenal, ambapo alikuwa anapiga pasi zilizomaliza mechi na kumfanya mchambuzi wa Sky Sports, Gary Neville kumtaja kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, ambayo The Gunners ilikubali kichapo cha mabao 3-1.

Utamu kimataifa

Wiki hii, akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa, Eriksen aliendelea moto wake na kuonyesha kwamba habatishi. Akikamatia kiungo kwenye mchezo dhidi ya mabingwa wa dunia Ufaransa, alitawala eneo hilo alipowafunika kabisa makinda na viungo wa kutegemewa wa Real Madrid, Eduardo Camavinga na Aurelien Tchouameni. Eriksen aligusa mpira mara 80, alipiga pasi muhimu nane na kupiga zaidi ya nusu ya krosi zote za Denmark. Hakupoteza mpira wowote uliokuwa kwenye miguu, huku pasi alizopiga zilikuwa sahihi kwa asilimia 84. Hapo hujazungumzia mpira alitengeneza wakati Denmark inatengeneza bao la kwanza lililofungwa na Kasper Dolberg au kona yake iliyosababisha bao la pili la Andreas Skov Olsen. Pasi nane muhimu alizopiga ndani ya mchezo huo zimeweka rekodi kwenye Nations League huku kiwango chake cha uwanjani kikimwagiwa sifa nyingi na kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps, aliposema: “Siku zote amekuwa na uwezo mkubwa wa kiufundi.” Huyo ndiye Christian Eriksen, tuendelee kutazama filamu inayoishi.