EPL pale juu ni weka niweke

Muktasari:

  • Nani atafanikiwa kuondoka na mwali wa Ligi Kuu England msimu huu? Ni Manchester City ambao ni mabingwa watetezi. Ni Liverpool au Arsenal? Mambo ni matamu na vita ni kali.

LONDON, ENGLAND: Moto uleule kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England msimu huu. Macho yote kwenye ubingwa.

Nani atafanikiwa kuondoka na mwali wa Ligi Kuu England msimu huu? Ni Manchester City ambao ni mabingwa watetezi. Ni Liverpool au Arsenal? Mambo ni matamu na vita ni kali.

Ukichungulia kwenye msimamo, Arsenal ipo namba moja baada ya kukusanya pointi 71 katika mechi 31, sawa na ilivyo kwa Liverpool kwenye nafasi ya pili, nao wamekusanya pointi 71 kwenye idadi kama hiyo ya mechi 31.

Namba tatu ni Man City wao wamekusanya pointi 70 katika mechi 31. Kwa maana hiyo, kila timu imebakiza mechi saba za kuamua vita hiyo ya kuwania taji la msimu huu. Nani atabeba?

Wikiendi hii moto unaendelea, ambapo kwenye orodha hiyo ya wanaowania ubingwa, Man City itakuwa ya kwanza kurusha kete yake wakati itakapojimwaga Etihad kuikabili Luton Town, iliyopo kwenye vita kali ya kukwepa kushuka daraja.

Ushindi kwa Man City utaifanya kushika usukani wa ligi hiyo na baada ya hapo itakuwa inasubiri matokeo ya wapinzani wake kwenye mchakamchaka huo.

Man City na Luton Town itakuwa mechi yao ya pili kukutana kwenye Ligi Kuu England, ambapo katika mchezo wa kwanza, jeshi la Pep Guardiola lilishinda 2-1 ugenini. Nini kitatokea hii leo Jumamosi, jeshi hilo la Man City litakapokuwa nyumbani Etihad kusaka pointi za kufukuzia ubingwa? Ngoja tuone.

Man City ikishinda, itajifariji kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi mbili. Lakini, itakapofika kesho, Jumapili inaweza kung’oka kwenye kilele endapo kama Liverpool itaibuka na ushindi kwenye mchezo wake dhidi ya Crystal Palace utakaopigwa uwanjani Anfield. Vita ni kali.

Liverpool na Palace zimekutana mara 29 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi tano zilimalizika kwa sare, huku vijana wa Jurgen Klopp wakiibuka na ushindi mara 19, tisa kwenye uwanja wao wa nyumbani na 10 ugenini, wakati Palace yenyewe imeshinda tano tu, mbili nyumbani na tatu ugenini.

Rekodi zinaonyesha kwamba kila timu imeshinda mechi moja zaidi ugenini kuliko nyumbani, hivyo kitakachokwenda kutokea Anfield kitakuwa na upinzani mkali kwelikweli.

Ushindi kwa Klopp na chama lake utawafanya kushuka usukani wa ligi, kwa muda kabla ya Arsenal haijamalizana na Aston Villa huko Emirates.

Uzuri wa wikiendi hii ni kwamba vigogo wote kwenye mbio za ubingwa wanacheza nyumbani. Arsenal itacheza na Aston Villa, inayonolewa na kocha wake wa zamani, Unai Emery. Patakuwaje hapo?

Namba zinaonyesha kwamba huu utakuwa mchezo wa 58 kwa Arsenal na Aston Villa kumenyana kwenye Ligi Kuu England, ambapo kwenye mechi 57 zilizopita, Arsenal imeshinda 31, mara 17 nyumbani na 14 ugenini, huku Aston Villa ikishinda 12, sita nyumbani na sita nyingine ugenini. Mechi 14 baina yao zilimalizika kwa sare. Mchezo wao wa mwisho kukutana kwenye ligi hiyo, Aston Villa ilishinda 1-0 Villa Park. Je, Emery atatibua mambo Emirates?

Ushindi wa Mikel Arteta na vijana wake wa Arsenal utawafanya kurejea kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo yenye upinzani mkali kabisa kwa msimu huu.

Kwenye vita ya Top Four, Tottenham Hotspur itakuwa ugenini St. James’ Park kukipiga na Newcastle United katika mechi inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali.

Kipute hicho kitapigwa leo Jumamosi, hivyo Aston Villa inayoshindania pia kwenye Top Four itakuwa imeshapata matokeo kabla ya kumalizana na Arsenal huko Emirates, hivyo ni jambo litakaloweza kuongeza upinzani kwenye mechi ya Arsenal. Mambo ni vuta nikuvute.

Newcastle na Spurs zimekutana mara 57 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi nane zilimalizika kwa sare, huku Spurs ikishinda 25, mara 16 nyumbani na tisa ugenini, wakati Newcastle yenyewe imeshinda 24, mara 13 nyumbani na 11 ugenini. Takwimu hizo zinaonyesha jinsi upinzani ulivyo kwa timu hizo za Newcastle na Spurs zinapokutana.

Mechi nyingine zitakazopigwa leo Jumamosi, Brentford itakuwa nyumbani kucheza na Sheffield United, wakati Burnley itakuwa na shughuli pevu na Brighton, huku Nottingham Forest itakuwa na kasheshe zito mbele ya Wolves. Ni moto juu ya moto.

Manchester United kwenye mwendo wa kusuasua itakuwa ugenini kukipiga na Bournemouth. Kipute hicho cha Vitality kitatoa taswira kwa vijana wa Erik ten Hag, Man United kama watakuwa bado wapo hai kwenye mbio za kuisaka Top Four ya Ligi Kuu England msimu huu ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Takwimu zinaonyesha kwamba huu utakuwa mchezo wa 14 kwa Bournemouth na Man United kukutana kwenye Ligi Kuu England, ambapo kwenye mechi 13 zilizopita, Man United imeshinda tisa, tano ikiwa nyumbani na nne ugenini, huku Bournemouth yenyewe imeshinda tatu, mbili nyumbani na moja ugenini. Mechi moja timu hizo zilitoka sare.

Mchezo mwingine wa kesho, Jumapili, West Ham United itakuwa nyumbani kucheza na Fulham kwenye kipute cha London derby. Fulham na West Ham zimekutana mara 27, ambapo katika mechi hizo, sita zilikuwa sare, huku Fulham ikishinda tano tu, nne nyumbani na moja ugenini, wakati West Ham imeshinda 16, ikishinda nane nyumbani na nane ugenini. Mambo ni moto kwelikweli.

Chelsea itasubiri hadi Jumatatu itakapojitupa Stamford Bridge kukipiga na Everton katika mechi inayotazamiwa kuwa kali kabisa. Everton inajaribu kukimbia kwenye hatari ya kushuka daraja na hicho ndicho kinachozidisha upinzani kwenye mchezo huo wa darajani.

Namba zinaonyesha, miamba hiyo imekutana mara 63 kwenye Ligi Kuu England, ambapo sare ni 21, huku Chelsea ikishinda 28, mara 17 nyumbani na 11 ugenini, wakati Everton imeshinda 14, mara 13 nyumbani na moja tu ugenini. Miamba hiuyo miwili yote inafahamika kama The Blues.