Endrick ruksa kuondoka Real Madrid
Muktasari:
- Endrick amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na klabu kadhaa za Ligi Kuu England ambazo zinaona bado ana nafasi kubwa ya kukua na kuwa nyota mkubwa barani Ulaya.
REAL Madrid inaangalia uwezekano wa kumuuza mshambuliaji wao chipukizi raia wa Brazil, Endrick mwenye umri wa miaka 19, mara atakaporejea kutoka kwa mkopo Olympique Lyon.
Endrick amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na klabu kadhaa za Ligi Kuu England ambazo zinaona bado ana nafasi kubwa ya kukua na kuwa nyota mkubwa barani Ulaya.
Real Madrid inaelewa kuwa fundi huyu anaweza kuwa tegemeo siku za usoni, lakini inataka kumuuza kwa pesa nyingi ambazo pia itazitumia kufanya usajili wa wachezaji wengine mwisho wa msimu.
Chelsea na Arsenal ni kati ya timu zinazotamani sana huduma ya staa huyu zikiwa zimevutiwa zaidi na uwezo mkubwa aliouonyesha akiwa Ligue 1 msimu huu.
Tangu atue Lyon, Endrick amecheza mechi sita za michuano yote na kufunga mabao matano, kiwango ambacho hakuwahi kukionyesha akiwa na Madrid.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030 na ripoti zinadai mabosi wa Madrid wanahitaji zaidi ya Pauni 70 milioni ili kumuuza staa huyu.
Madrid inaamini Endrick ana uwezo mkubwa, lakini hata akirudi katika kikosi chao itakuwa ngumu kupata nafasi ya kucheza katika safu yao ya ushambuliaji.
Murillo
NOTTINGHAM FOREST huenda ikampoteza beki wake wa kati Murillo, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, baada ya Chelsea na Liverpool kuonyesha nia ya kumsajili.
Murillo, ambaye ni raia wa Brazil, amekuwa mmoja wa wachezaji wanaohitajika na timu nyingi barani Ulaya tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini Forest iligoma kumuuza kwa wakati huo.
Chelsea inamtazama mkali huyu kama sehemu ya mpango wa wa kujenga safu mpya ya ulinzi ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwa msimu ujao.
Scott McTominay
NAPOLI imeanza mazungumzo rasmi na wawakilishi wa kiungo wake wa kimataifa wa Scotland, Scott McTominay, 29, ili kumuongeza muda wa mkataba wake hadi mwaka 2030.
McTominay ameonekana kuzoea haraka maisha ya soka la Italia tangu ajiunge na Napoli, akitoa mchango mkubwa katika safu ya kiungo hata akapewa tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa kikosi chao katika msimu wake wa kwanza.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 38 za michuano yote na kufunga mabao 10.
Morgan Gibbs-White
MANCHESTER City imeambiwa kuwa italazimika kulipa kati ya Pauni 60 hadi 70 milioni ili kuinasa saini ya kiungo wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya England, Morgan Gibbs-White, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Gibbs-White amekuwa nguzo muhimu Forest msimu huu lakini Man City inataka kumchukua ili akawe mbadala wa baadhi ya wachezaji wao wanaotarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu. Mkataba wa sasa wa Morgan unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Kim Min-jae
CHELSEA na Tottenham Hotspur zimeonyesha nia ya kumsajili beki wa kati wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Korea Kusini, Kim Min-jae, 29.
Kim Min-jae ana uzoefu mkubwa wa soka la ushindani barani Ulaya na amewahi kung'ara Serie A kabla ya kujiunga na Bayern.
Chelsea inaamini Kim ana uzoefu ambao utasaidia sana wachezaji wao vijana katika safu ya ushambuliaji.
Bayern haijaonyesha dalili yoyote ya kuwa tayari kumwachia kirahisi. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Yan Diomande
WINGA wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yan Diomande, 19, ameweka wazi kuwa Liverpool ni klabu ambayo baba yake anaishabikia, jambo lililozidisha tetesi za chipukizi huyo kuhamia Anfield katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Hata hivyo, mbali ya Liverpool, saini ya Diomande inahitajika pia na Bayern Munich ambayo haipo tayari kuona ikimkosa.
Kocha wa Bayern, Vincent Kompany ni shabiki mkubwa wa mchezaji huyu.
Harry Wilson
EVERTON inapanga kufanya jaribio jingine la kumsajili winga wa kimataifa wa Fulham na timu ya taifa ya Wales, Harry Wilson, 28, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya ofa yao katika dirisha lililopita kugonga mwamba.
Klabu hiyo ya Goodison Park iliwahi kuwasilisha ofa kwenda Fulham, lakini ikakataliwa, jambo linalowafanya kujiandaa kwa ajili ya kupeleka ofa mpya mwisho wa msimu ambapo mkataba wa Harry utakuwa unamalizika.
Christian Pulisic
MANCHESTER United na Arsenal zimeonyesha nia ya kumrudisha Ligi Kuu England mshambuliaji wa AC Milan na timu ya taifa ya Marekani, Christian Pulisic, 27, huku Tottenham Hotspur pia ikiwa kwenye mbio hizo.
Pulisic, ambaye aliwahi kucheza Chelsea anaonekana kuimarika zaidi akiwa Serie A, hali iliyozivutia tena klabu za England. Inaripotiwa kuwa staa huyo anauzwa kwa kiasi kisichopungua Euro 70 hadi 80 milioni.
Mbali ya Man United na Arsenal, saini ya fundi huyu pia inawindwa na Tottenham.
Hata hivyo, Milan haina presha ya kumuuza mapema, na uamuzi wa mwisho utategemea ofa itakayowasilishwa pamoja na msimamo wa Pulisic mwenyewe kuhusu mustakabali wake.