Endrick apata habari njema, kuitwa baba
Muktasari:
- Akiwa Lyon, Endrick alianza vizuri akifunga hat-trick kwenye ushindi wa mabao 5–2 dhidi ya FC Metz na kwa ujumla amefunga mabao sita na kutoa asisti tano, ingawa amekuwa kimya katika wiki za karibuni.
LYON, UFARANSA: NYOTA chipukizi wa Real Madrid, Endrick Felipe Moreira de Sousa maarufu kama Endrick (19), anayecheza kwa mkopo Olympique Lyon ya Ufaransa na mkewe Gabriely Miranda (23), wametangaza kuwa wanatarajia kupata mtoto wa kwanza.
Wanandoa hao wametoa habari hiyo kupitia mitandao ya kijamii, huku Miranda akichapisha video na picha zikionyesha furaha yao akisema: “Sasa tupo watano.”
Miranda aliandika hayo akimaanisha wao wawili, mtoto anayetarajiwa pamoja na mbwa wao wawili, huku akiongeza pia nukuu ya Biblia kutoka Zaburi 139:13 isemayo: “Wewe ulinisuka tumboni mwa mama yangu.
Endrick na Miranda walifunga ndoa Septemba 2024, chini ya mwaka mmoja baada ya kuanza uhusiano na wawili hao pia walifichua kuwa waliweka “mkataba wa uhusiano” wenye masharti kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutojiingiza kwenye uraibu wowote, kusema “nakupenda” kila wakati na kudumisha heshima, kuelewana na mapenzi.
Taarifa zinasema pia mkataba huo ulijumuisha Endrick kutoruhusiwa kuwa na “mpenzi wa mtandaoni” ndani ya Grand Theft Auto V pamoja na kuto-komenti picha za wasichana wengine kwenye mitandao ya kijamii.
Miranda alihamia Hispania kumfuata mumewe baada ya Endrick kujiunga na Real Madrid kwa Pauni 51 milioni akitokea Palmeiras majira ya joto 2024. Baadaye, Desemba, Endrick alihamia Ufaransa kwa mkopo kujiunga na Olympique Lyon ili kupata muda zaidi wa kucheza.
Akiwa Lyon, Endrick alianza vizuri akifunga hat-trick kwenye ushindi wa mabao 5–2 dhidi ya FC Metz na kwa ujumla amefunga mabao sita na kutoa asisti tano, ingawa amekuwa kimya katika wiki za karibuni.
Kocha wa Lyon, Paulo Fonseca, alimkosoa Endrick kwa kusema anahitaji kufanya zaidi ili kuisaidia timu baada ya kipindi kigumu cha mechi tisa bila ushindi. Endrick pia alicheza mechi za wiki mbili zilizopita za kimataifa akiichezea timu ya taifa ya Brazil ilipokuwa Marekani, na alidai uchovu wa safari ulichangia kushindwa kuonyesha kiwango kizuri katika suluhu dhidi ya Angers majuzi katika mechi ya Ligi Kuu Ufaransa.