Emiliano Martinez ‘achizika’ na ubingwa Europa League
Muktasari:
- Kipyenga cha mwisho kilipopulizwa, kipa huyo raia wa Argentina alianguka kwa magoti na kushika kichwa chake kwa mshtuko wa furaha, kabla ya kuelekea jukwaani kujumuika na mashabiki wa Villa waliokuwa wakishangilia kwa furaha.
KIPA wa Aston Villa, Emiliano 'Emi' Martinez, alishindwa kuzuia hisia zake na kuangua kilio cha furaha baada ya kikosi hicho kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Freiburg katika fainali ya Europa League mjini Istanbul, jana Jumatano, Mei 20, 2026.
Kipyenga cha mwisho kilipopulizwa, kipa huyo raia wa Argentina alianguka kwa magoti na kushika kichwa chake kwa mshtuko wa furaha, kabla ya kuelekea jukwaani kujumuika na mashabiki wa Villa waliokuwa wakishangilia kwa furaha.
Wachezaji wenzake walijawa na furaha isiyo na kifani uwanjani hapo huku klabu hiyo ya Midlands ikijikatia tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Machozi ya kipa huyo raia wa Argentina yana maana kubwa kwani amekuwa na klabu hiyo kwa miaka sita, na hili ndilo taji lake la kwanza kufanikiwa kulitwaa katika kipindi chote cha utumishi wake.
Hisia hizo zinaeleweka vizuri ukizingatia kuwa mwishoni mwa msimu uliopita, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alionekana akilia kwa uchungu akiamini kuwa ameshacheza mechi yake ya mwisho klabuni hapo kutokana na uvumi mkubwa uliokuwepo kuwa angeondoka wakati wa majira ya kiangazi.
Hata hivyo, aliamua kubaki na sasa amekuwa nguzo muhimu katika lango la Aston Villa na kupata mafanikio ya ubingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu miaka ya 1980.
Katika mchezo huo wa fainali, vijana wa kocha Unai Emery walionyesha soka la kiwango cha juu sana na kutawala mchezo dhidi ya wapinzani wao kutoka Ujerumani.
Youri Tielemans alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 40 kwa mkwaju mkali uliotokana na shambulizi lililosukwa kwa ufundi mkubwa na kuwapa Villa mwelekeo mzuri wa mchezo.
Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, Emi Buendia aliongeza bao la pili kwa shuti kali la mguu wa kushoto lililotinga moja kwa moja kwenye kona ya juu ya lango na kuzidisha presha kwa Freiburg.
Kipindi cha pili kilipoanza, Aston Villa iliendelea kulisakama lango la wapinzani wao hadi pale Morgan Rogers alipofunga bao la tatu na la mwisho dakika ya 57.
Freiburg ilionekana kukata tamaa na haikuonyesha dalili zozote za kuweza kurudi mchezoni kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Villa iliyokuwa chini ya Martinez. Ushindi huu unaweka historia mpya kwa Aston Villa huku ikirejea kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya 2024–2025 kuishia robo fainali.