Emery kuikazia Arsenal kwa Watkins
Muktasari:
- Ushindi wa 4-2 dhidi ya Celtic uliwahakikishia Villa nafasi katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa, lakini siku hiyo ilikumbwa na sintofahamu kuhusu mustakabali wa washambuliaji wao wawili.
BIRMINGHAM, ENGLAND: LICHA ya Arsenal kuwa na matumaini makubwa ya kuipata saini ya Ollie Watkins, Kocha wa Aston Villa, Unai Emery amedhamiria kumbakisha baada ya Jhon Duran kuwa katika hatua za mwisho kuuzwa Al Nassr.
Ushindi wa 4-2 dhidi ya Celtic uliwahakikishia Villa nafasi katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa, lakini siku hiyo ilikumbwa na sintofahamu kuhusu mustakabali wa washambuliaji wao wawili.
Emery alithibitisha Duran anakaribia kuhamia Al Nassr kwa dau linalokaribia Pauni 63 milioni na inadaiwa alifanya vipimo vya afya London Alhamisi.
Wakati dili la Duran likiwa hatua za mwisho kukamilika, Villa ilipigwa butwaa baada ya Arsenal kuwasilisha ofa kwa Watkins saa chache kabla ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa kuanza.
Awali Emery alidai kila mchezaji kwenye kikosi chao anaweza kuuzwa ikiwa itapatikana ofa sahihi.
"Sitaki kuona akiuzwa, kwa dili lolote, tutakuwa wagumu sana. Ollie Watkins ni mshambuliaji wetu. Kuna uvumi mwingi kuhusu wachezaji wetu, lakini muhimu zaidi ni jinsi wanavyojibu uwanjani. Wanatuonyesha ni wakomavu na wanawajibika, kuhusu Jhon Duran. Ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa. Nilimtaka hapa, lakini anataka nini? Kila mtu ana malengo tofauti na tunapaswa kuheshimu hilo," alisema Emery.
"Ikiwa anaondoka (Duran), ni kwa sababu anataka kuchukua njia nyingine katika maisha yake ya soka. Hili ni jambo zuri kwa klabu kwa sababu tumempandisha thamani kwa miaka miwili iliyopita," aliongeza.
"Ni habari njema kupata ofa kutoka timu nyingine juu ya wachezaji wetu, lakini sisi tunataka kudumisha malengo yetu kwa mastaa tulionao. Kubaki kwenye kiwango tulichofikia ndiyo changamoto kubwa zaidi iliyo mbele yetu."