Emery adai Rashford yupo moto mazoezini
Muktasari:
- Fowadi huyo amejiunga kwa mkopo Aston Villa akitokea Manchester United, ambako hakucheza mechi yoyote tangu Desemba kwa madai ya Kocha Ruben Amorim hakuwa akionyesha kiwango bora mazoezini.
BIRMINGHAM, ENGLAND: KOCHA wa Aston Villa, Unai Emery amesema amevutiwa na kiwango cha mazoezi ya mchezaji Marcus Rashford hivyo kuna uwezekano mkubwa akampa nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi watakapokabiliana na Tottenham Hotspur leo Jumapili.
Fowadi huyo amejiunga kwa mkopo Aston Villa akitokea Manchester United, ambako hakucheza mechi yoyote tangu Desemba kwa madai ya Kocha Ruben Amorim hakuwa akionyesha kiwango bora mazoezini.
Rashford, 27, aliwekwa nje ya kikosi cha Man United kwa muda mrefu na hivyo kumfanya mwenyewe kufunguka kwamba yupo tayari kwenda kukabiliana na changamoto mpya nje ya Old Trafford.
Baada ya kuhusishwa na klabu za Borussia Dortmund, Barcelona na AC Milan, hatimaye Rashford alikwenda kujiunga na Aston Villa kwa mkopo kwenye dirisha la usajili wa Januari na miamba hiyo ya Villa Park inaweza kumbeba jumla mwisho wa msimu endapo kama itakubali kulipa Pauni 40 milioni.
Kocha Emery alisema anavutiwa na kiwango cha Rashford
alichoonyesha mazoezini na kwamba huenda akampa nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza.
"Leo (Ijumaa) amefanya mazozini vizuri sana, kesho tena na Jumapili (leo) ni mechi," alisema Emery.
"Tutafurahia kila hatua na baada ya hapo, hatima ya kila kitu hujengwa kuanzia sasa."
Bosi huyo wa Aston Villa alibainisha kuwa na furaha kubwa baada ya kumjuimisha Rashford kwenye kikosi chake huku dhamira yake kubwa ikiwa kumfanya mkali huyo wa kimataifa wa England kufikia mafanikio makubwa kwenye mchezo wa soka.
Kocha wa Man United, Amorim alisema: "Namtakia kila la heri Rashford na kocha Unai Emery, wanaweza kuwa na muunganiko mzuri."