Duh! Terry kapitia wakati mgumu sana
Muktasari:
- Nahodha huyo wa zamani wa Chelsea amengeipa ubingwa wa taji hilo la Ligi ya Mabingwa Ulaya timu yake endapo kama mkwaju wake wa penalti ungetinga kwenye nyavu za Man United.
LONDON, ENGLAND: BEKI wa boli, John Terry amefunguka msongo wa mawazo uliomkabili kiasi cha kufikiria kujitoa uhai baada ya kukosa penalti katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Chelsea na Manchester United iliyofanyika Moscow, 2008.
Nahodha huyo wa zamani wa Chelsea amengeipa ubingwa wa taji hilo la Ligi ya Mabingwa Ulaya timu yake endapo kama mkwaju wake wa penalti ungetinga kwenye nyavu za Man United.
Lakini, aliteleza kabla ya kupiga mkwaju huo na hivyo mpira ukagonga mwamba kuipa nafasi Man United kwenda kunyakua taji hilo baada ya mikwaju hiyo kufikia kwenye hatua ya penalti moja moja piga nikupige.
Terry alihitaji kutulizwa sana kiakili baada ya kukosa mkwaju wake wa penalti ambao ungeifanya Chelsea kushinda taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na sasa amefichua kilichotokea baada ya hapo baada ya kurudi chumbani kwake kwenye hoteli moja iliyokuwa imefikia timu ya Chelsea huko Moscow.
Terry alisema: “Baada ya mechi, tulirudi hotelini na mimi nilikuwa kwenye ghorofa ya 25. Nilikuwa nasogelea dirishani na kujiuliza maswali mengi akilini mwangu, 'kwa nini?, kwa nini lakini?'. Sisemi kama ningepata nafasi ya kujirusha ningejirusha, lakini ni kitu ambacho kilikuwa kikipita akilini kwa wakati ule.
“Kisha wachezaji wenzangu walikuja na kunishusha chini. Hizo ni nyakati za ‘ingekuwa vipi?’ nyakati ambazo hupati picha.”
Terry aliitumikia Chelsea kwa miaka tisa na hatimaye alipata nafasi ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012. Lakini, alishindwa kucheza mechi ya fainali baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye hatua ya nusu fainali.
Terry alishinda mataji matano ya Ligi Kuu England na mataji mengine kibao kwa wakati wake aliokuwa Chelsea.