Dowman aweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kucheza UEFA
Muktasari:
- Akiwa na miaka 15 na siku 308, kinda huyo amevunja rekodi iliyowekwa na Youssoufa Moukoko, ambaye aliichezea Borussia Dortmund dhidi ya Zenit akiwa na miaka 16 na siku 18.
PRAGUE, CZECH: KINDA wa Arsenal, Max Dowman, ameweka rekodi mpya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba katika ushindi wa 0–3 dhidi ya Slavia Prague ugenini nchini Jamhuri ya Czech, Novemba 4, 2025.
Akiwa na miaka 15 na siku 308, kinda huyo amevunja rekodi iliyowekwa na Youssoufa Moukoko, ambaye aliichezea Borussia Dortmund dhidi ya Zenit akiwa na miaka 16 na siku 18.
Dowman aliingia uwanjani dakika ya 72 kuchukua nafasi ya Leandro Trossard, wakati Arsenal iliposhinda mechi ya 10 mfululizo na clean sheet ya nane mfululizo, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa usiku wa Jumanne Novemba 4, 2025, rekodi ambayo haikuwahi kurudiwa na klabu hiyo tangu mwaka 1903.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amemiminia sifa nyingi kijana huyo akisema: “Hakuna mashindano magumu kama haya, na Max, akiwa na miaka 15 tu, aliingia uwanjani akionyesha ujasiri, akiwapiga chenga watu na kupata faulo. Ana kipaji cha ajabu katika muda sahihi wa kutoa mpira. Tuna mchezaji mkubwa sana hapo.”
Rekodi hii ya Dowman imekuja siku sita tu baada ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuanza mechi kwa Arsenal katika ushindi wa Kombe la EFL dhidi ya Brighton.
Winga huyo tayari ndiye mchezaji wa pili mdogo zaidi kuwahi kuichezea Arsenal na wa pili mdogo zaidi kucheza Ligi Kuu ya England, rekodi zote mbili zikishikiliwa na Ethan Nwaneri, ambaye alicheza akiwa na miaka 15 na siku 181.
WACHEZAJI WADOGO ZAIDI KUCHEZA UEFA:
1. Max Dowman (Arsenal) – miaka 15 na siku 308, (Novemba 4, 2025
2. Youssoufa Moukoko – miaka 16 na siku 18, (Desemba 8, 2020)
3. Lamine Yamal (Barcelona) – miaka 16 na siku 68, Septemba 19, 2023)
4. Celestine Babayaro (Anderlecht) – miaka 16 na siku 86, (Novemba 23, 1994)
5. Rayan Cherki (Lyon) – miaka 16 na siku 102, (Novemba 27, 2019)