Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Doue ang’ara PSG ikishinda saba kwa Leverkusen

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo iliyochezwa usiku wa Oktoba 21, 2025 pale BayArena, Desire Doue alifunga mara mbili, huku Willian Pacho na Khvicha Kvaratskhelia wakiongeza mabao mengine kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika na PSG kuongoza 4-1. Nuno Mendes, mshindi wa Ballon d’Or Ousmane Dembele na Vitinha walikamilisha kipigo hicho kikali.

LEVERKUSEN, UJERUMANI: Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris Saint-Germain wametoa onyo kali baada ya kuibamiza Bayer Leverkusen mabao 2-7 na kufikisha ushindi wa tatu mfululizo katika michuano hiyo.

Katika mechi hiyo iliyochezwa usiku wa Oktoba 21, 2025 pale BayArena, Desire Doue alifunga mara mbili, huku Willian Pacho na Khvicha Kvaratskhelia wakiongeza mabao mengine kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika na PSG kuongoza 4-1. Nuno Mendes, mshindi wa Ballon d’Or Ousmane Dembele na Vitinha walikamilisha kipigo hicho kikali.

Beki Willian Pacho aliipa PSG bao la kuongoza dakika ya saba baada ya kukutana na krosi murua ya Nuno Mendes. Dakika 16 baadaye, Leverkusen ilipata penalti baada ya Illia Zabarnyi kumchezea rafu Claudio Echeverri.

Hata hivyo, mkwaju wa Alejandro Grimaldo uligonga mwamba, na dakika saba baadaye nahodha wa Leverkusen, Robert Andrich, alionyeshwa kadi nyekundu baada ya VAR kubadilisha kadi ya njano kufuatia kumgonga Doue usoni kwa kiwiko.

Faida ya kuwa na mchezaji mmoja zaidi haikudumu muda mrefu kwa PSG, kwani Zabarnyi naye alitolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumuangusha Christian Kofane ndani ya eneo la penalti.

Mashabiki wa Leverkusen walishangilia Aleix Garcia alipofunga penalti hiyo, lakini furaha yao haikudumu. Ndani ya dakika tano pekee, Doue alifunga kwa mkwaju wa chini uliopinda, Kvaratskhelia akaongeza kwa shuti lililogonga miamba yote miwili kabla ya kuingia wavuni, na Doue akamalizia shambulizi la kushtukiza kwa mkwaju wa kupinda.

Kipindi cha pili kilianza kwa mtindo huohuo, Vitinha alipenya katikati ya safu ya kiungo ya Leverkusen na kumpasia Mendes aliyemalizia kwa ustadi kwenye lango la Mark Flekken.

Garcia alipunguza bao kwa shuti kali la umbali wa yadi 30 lililopaa hadi kona ya juu ya lango, lakini Dembele, aliyekuwa amerudi kutoka kuuguza majeraha ya misuli, aliifungia PSG bao la sita dakika tatu tu tangu aingie uwanjani.

Vitinha alikamilisha bao la saba dakika ya 90, akipiga shuti la chini lililokwenda moja kwa moja kwenye kona ya lango.