Dili la Mbeumo bado halijaeleweka
Muktasari:
- Newcastle United ilimweka kwenye rada zake kwa muda mrefu fowadi huyo aliyefunga mabao 20 kwenye ligi msimu uliopita, lakini kinachoelezwa hawezi kwenda St James’ Park.
LONDON, ENGLAND: SWALI moja gumu, Bryan Mbeumo anakwenda wapi? Staa huyo wa Brentford amejikuta kwenye sintofahamu kubwa wakati huu akisakwa na vigogo wa Ligi Kuu England katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Newcastle United ilimweka kwenye rada zake kwa muda mrefu fowadi huyo aliyefunga mabao 20 kwenye ligi msimu uliopita, lakini kinachoelezwa hawezi kwenda St James’ Park.
Kwa mujibu wa taarifa za kutoka Newcastle, dili hilo limekwama kwa sababu Brentford inataka pesa nyingi, huku mshahara pia ukitajwa kuwa tatizo. Lakini, pia mchezaji huyo akidaiwa hataki kwenda Kaskazini Mashariki.
Na badala yake, chaguo lake la kwanza lilikuwa Manchester United, mahali ambako anatazamwa kama kipaumbele kwenye usajili huu baada ya kumchukua staa wa Wolves, Matheus Cunha. Man United imepeleka ofa, lakini ilikuwa pungufu ya kiwango ambacho Brentford inahitaji, kwani miamba hiyo ya Old Trafford iliweka ubaoni ofa ya Pauni 45 milioni kwanza, kisha itaongeza Pauni 10 milioni, ambayo ilikataliwa, kabla ya kupeleka ofa nyingine iliyokataliwa pia.
Lakini, sasa Tottenham imeibuka na kutaka kuipora Man United dili hilo la Mbeumo baada ya kocha wao mpya, Thomas Frank kutaka kuungana na mchezaji wake huyo anayemfahamu vyema. Na kinachoelezwa, Spurs imeweka mkwanja mrefu mezani ili kumpata Mbeumo.
Spurs imeweka ofa ya Pauni 70 milioni, ambapo itatanguliza Pauni 65 milioni na Pauni 5 milioni italipa baadaye. Kiasi hicho ni zaidi kwa Pauni 10 milioni ya ofa ya mwisho ya Man United. Kinachoelezwa, Mbeumo mwenyewe anataka kwenda Man United. Ofa tamu ya mshahara huko Old Trafford, itashuhudiwa akilipwa kati ya Pauni 150,000 na Pauni 175,000 kwa wiki, ukiweka na bonasi, basi Mbeumo anaweza kuchukua Pauni 200,000 kwa wiki.
Kwenye mshahara, Spurs haiwezi kushindana ubavu na Man United, ambapo Mbeumo akienda huko basi atarajie kulipwa kati ya Pauni 130,000 na Pauni 140,000 kwa wiki, hata kwa bonasi bado atakuwa chini ya ofa ya Old Trafford. Jambo hilo ndilo linaloibua swali hili, Mbeumo atakwenda wapi?