Dili la Haaland lashusha presha mabeki England

Dili la Haaland lashusha presha mabeki England

MANCHESTER, ENGLAND. MABEKI wa Ligi Kuu England watashusha pumzi maana balaa litawaondoka. Ndicho unachoweza kusema baada ya Erling Haaland kuripotiwa kwamba mkataba wake Manchester City una kipengele cha kumruhusu kwenda Real Madrid itakapofika mwaka 2024.
Straika Haaland, 22, yupo moto kwelikweli kwenye Ligi Kuu England akifunga hat-trick yake ya tatu msimu huu wakati chama lake la Man City lilipoangusha kipigo kizito kwa mahasimu wao Manchester United cha mabao 6-3 Jumapili iliyopita.
Mabao hayo yamemfanya Haaland kufikisha 17 katika mechi 10 alizocheza tangu alipotua Man City akitokea Borussia Dortmund.
Alipotua Etihad alisaini mkataba wa miaka mitano utakaofika tamati 2027, baada ya kunaswa kwa Pauni 51 milioni Juni, 2022.
Kwenye usajili wake vita ilikuwa kali kutoka kwa Real Madrid na Barcelona, lakini Haaland aliamua kwenda kuwa chini ya kocha Pep Guardiola huko Etihad na mambo yake yamekuwa mazuri kwelikweli kwenye Ligi Kuu England.
Hata hivyo, kumeibuka ripoti kwamba ndani ya wiki chache tu baada ya kumsajili, Man City inajaribu kufanya mchakato wa kumsainisha mshambuliaji huyo mkataba mpya wenye nguvu zaidi. Ripoti zinafichua kwamba Man City wanafahamu wazi mshambuliaji huyo atakwenda zake Hispania ndani ya miaka michache ijayo na Fernando Sanz, mchezaji wa zamani wa Real Madrid na rais wa zamani wa  klabu ya Malaga, alisema Los Blancos watamnasa 2024.
Sanz aliambia MundoDeportivo: "Taarifa nilizonazo kuna kipengele kinachomruhusu Haaland kuondoka kwenye mwaka wake wa pili na kuna timu itakuwa na faida kubwa kuliko klabu nyingine nao ni Real Madrid. Haaland aliweka kipengele cha kumruhusu kuondoka baada ya miaka miwili, lakini wanaopewa kipaumbele ni Real Madrid. Na hapo Madrid wataweka pesa inayohitaji kumchukua Haaland bila ya kuzungumza na Man City."
Na Alfie Haaland, ambaye ni baba wa mchezaji Haaland, aliyewahi pia kuichezea Man City, alisema mwanaye hajapanga kukaa kwa muda mrefu England, aliposema: “Erling anaweza kuwa amekaa miaka 2½ Ujerumani, miaka 2½ England, na kisha atakwenda Hispania, Italia, Ufaransa, sawa? Hatufahamu kama itakuwa hivyo, lakini nadhani atajaribu uwezo wake kwenye ligi kubwa.”