Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dias aipa Colombia ushindi, Cannavaro aanza kwa kichapo Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo, beki wa Crystal Palace ya England, Daniel Munoz ndiye aliyeanza kufungua akaunti ya mabao kwa Colombia dakika ya 40, akimalizia pasi nzuri ya Luis Dias na kuipeleka timu hiyo mapumziko ikiwa inaongoza.

MEXICO CITY, MEXICO: MABAO mawili aliyochangia leo mshambuliaji wa Bayern Munich ya Ujerumani, Luis Dias yametosha kuipa ushindi timu ya taifa ya Colombia wa mabao 3-1, dhidi ya Uzbekistan, katika mechi ya Kombe la Dunia kundi K, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azteca, Mexico City.

Katika mechi hiyo, beki wa Crystal Palace ya England, Daniel Munoz ndiye aliyeanza kufungua akaunti ya mabao kwa Colombia dakika ya 40, akimalizia pasi nzuri ya Luis Dias na kuipeleka timu hiyo mapumziko ikiwa inaongoza.

Kipindi cha pili kilianza kwa Colombia kuendelea kutawala mechi, ingawa dakika ya 60, ilishtushwa baada ya Uzbekistan kusawazisha bao hilo kupitia kwa Abbosbek Fayzullaev likiwa ni bao la kwanza kwa kikosi hicho katika historia ya Kombe la Dunia.

Dakika tano baadae, Colombia ikajibu mapigo na Dias aliiandikia bao la pili dakika ya 65, akimalizia pasi safi ya Gustavo Puerta likiwa ni bao lake la pili pia kuhusika baada ya kutoa asisti ya la kwanza.

Dakika ya 90+9, Colombia ikapata bao la tatu lililofungwa na Jaminton Leandro Campaz aliyemalizia pasi ya Cucho Hernandez na kumwacha Kocha Mkuu wa Uzbekistan, Fabio Cannavaro akianza vibaya kampeni za Kombe la Dunia.

Matokeo hayo yanaifanya Colombia kuongoza kundi K na pointi tatu, nyuma ya Ureno na DR Congo zenye pointi moja kila moja, baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, mechi ya kwanza ya ufunguzi, huku Uzbekistan ikishika mkiani bila ya pointi.

Colombia inayofundishwa na Kocha Mkuu, Nestor Lorenzo imerejea Kombe la Dunia baada ya kukosekana Qatar mwaka 2022, huku ikimaliza nafasi ya tatu ya mchujo ya Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (CONMEBOL), nyuma ya Argentina na Ecuador.

Timu hiyo maarufu kwa jina la 'Los Cafeteros' inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya saba tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1962, huku Kocha Lorenzo akikumbukwa kwa kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 1990, akiwa na Argentina.

Mafanikio makubwa kwa Colombia katika Kombe la Dunia tangu ishiriki ni kuishia hatua ya robo fainali, baada ya kuchapwa na wenyeji, Brazil mabao 2-1, Julai 4, 2014, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Castelao, uliopo Jiji la Fortaleza.

Katika fainali hizo za mwaka 2014, zitaendelea kubakia katika historia ya Colombia, kwani licha ya kufika robo fainali kwa mara ya kwanza, ila nyota wa timu hiyo, James Rodriguez aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao sita.

Kwa upande wa Uzbekistan inacheza kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia mwaka 2026, tangu taifa hilo lilipojitenga baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, huku timu hiyo ya Asia ya Kati ikibeba matumaini makubwa kwa mashabiki wao.

Timu hiyo maarufu kwa jina la 'White Wolves' (Mbwa Mwitu Weupe), iliandika rekodi mpya ya kufuzu Kombe la Dunia, Juni 5, 2025, baada ya suluhu (0-0), dhidi ya Falme za Kiarabu (UAE), ikishinda mechi 10, sare tano na kupoteza moja kati ya 16.

Uzbekistan inafundishwa na Kocha Fabio Cannavaro aliyewahi kuwa nahodha wa Italia na kushinda Kombe la Dunia mwaka 2006, akipewa jukumu hilo kubwa ili kuleta uzoefu katika timu hiyo.

Kabla ya Cannavaro kuteuliwa Oktoba 6, 2025, timu hiyo ilianza kampeni za kuisaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia kwa kufundishwa na makocha wawili akianza, Srecko Katanec kisha, Timur Kapadze aliyeondoka pia na kumwachia mikoba Muitaliano huyo.

Uwepo wa makocha hao wawili  Katanec na Kapadze ulichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya kikosi hicho na kimefuzu Kombe la Dunia 2026, baada ya kumaliza nafasi ya pili hatua ya makundi nyuma ya Iran. 

Licha ya uchanga wa timu hiyo katika michuano hiyo, miongoni mwa wachezaji waliobeba matumaini ya taifa hilo ni nahodha, Eldor Shomurodov aliyechangia mabao tisa ya kikosi hicho hatua ya kufuzu akiwa ndiye muhimili kikosini.

Mbali na Shomurodov anayeichezea Istanbul Basaksehir ya Uturuki kutegemewa katika ushambuliaji, ila nyota wa Manchester City ya England, Abdukodir Khusanov ni beki anayetegemewa kwenye eneo la safu ya kujilinda ya kikosi hicho.