Mastaa England wapongezwa kwa mabusu
Muktasari:
- Mara baada ya mchezo huo kumalizika, nyota wa England walipanda jukwaani kuungana na familia zao pamoja na wapenzi waliokuwa wamefika kuwapa sapoti katika mchezo huo.
ARLINGTON, TEXAS: BAADA ya England kuanza kwa kishindo fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Croatia, mastaa wa timu hiyo waliamua kusherehekea matokeo hayo pamoja na wapenzi wao.
Mara baada ya mchezo huo kumalizika, nyota wa England walipanda jukwaani kuungana na familia zao pamoja na wapenzi waliokuwa wamefika kuwapa sapoti katika mchezo huo.
Kiungo nyota wa England, Jude Bellingham, alikuwa miongoni mwa waliovuta macho ya wengi baada ya kuonekana akisherehekea ushindi huo pamoja na mpenzi wake, Ashlyn Castro.
Mrembo huyo kutoka Los Angeles alimkaribisha Bellingham kwa busu la mahaba huku wawili hao wakionekana kufurahia mwanzo mzuri wa England katika mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani.
Ashlyn ambaye ni mwanamitandao maarufu nchini Marekani, alikuwa amevaa jezi ya England wakati wote wa mchezo na aliketi karibu na wazazi wa Bellingham, Denise na Mark, wakishuhudia Three Lions ikitoa onyo kwa wapinzani wake.
Nahodha wa England, Harry Kane, naye alikuwa na sababu ya kutabasamu baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi huo.
Mara baada ya filimbi ya mwisho, Kane alionekana akisherehekea na mkewe, Katie Goodland ambaye alimpongeza kwa busu huku wakifurahia usiku mzuri uliowaacha mashabiki wa England wakiwa na matumaini makubwa.
Lakini wakati baadhi ya wake na wapenzi wa nyota hao wakifurahia ushindi huo, Megan Pickford, mke wa kipa wa England, Jordan Pickford.
Megan alifichua kuwa alipata mkasa mkubwa wakati akisafiri kuelekea Marekani baada ya mzigo wake kupotea njiani, hali iliyomwacha bila nguo nyingi alizokuwa amebeba kwa ajili ya safari hiyo.
Hata hivyo, tatizo hilo halikumzuia kufika Arlington kumuunga mkono mumewe.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Megan aliweka picha akiwa nje ya uwanja kabla ya mechi na kueleza kuwa hakuna tatizo ambalo lingeweza kumzuia kuwa upande wa Jordan katika mechi hiyo muhimu.