Ronaldo apotea, Messi na Mbappe wamfunika
Muktasari:
- Kabla ya mechi ya Ureno dhidi ya DR Congo, kila kitu kilionekana kuwa sawa kwa ajili ya nahodha huyo wa Ureno kuandika historia nyingine katika maisha yake ya soka. Akiwa na miaka 41, Ronaldo aliingia uwanjani akiwa na nafasi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika michuano sita tofauti ya Kombe la Dunia.
HOUSTON, MAREKANI: WAKATI katika michezo ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia 2026 yakishuhudiwa maajabu kutoka kwa nyota wakubwa wa soka duniani kwa Cristiano Ronaldo na imekuwa tofauti.
Kabla ya mechi ya Ureno dhidi ya DR Congo, kila kitu kilionekana kuwa sawa kwa ajili ya nahodha huyo wa Ureno kuandika historia nyingine katika maisha yake ya soka. Akiwa na miaka 41, Ronaldo aliingia uwanjani akiwa na nafasi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika michuano sita tofauti ya Kombe la Dunia.
Lakini badala ya kuandika historia, alijikuta akiondoka uwanjani akiandamwa na lawama huku Ureno ikishikwa shati kwa sare ya bao 1-1 na DR Congo katika moja ya matokeo ya kushtua katika hatua za awali za mashindano hayo.
Matokeo hayo yamezua mjadala kuhusu nafasi ya Ronaldo ndani ya kikosi cha Ureno, uwezo wake wa sasa na kama kocha Roberto Martinez anaendelea kumtegemea kwa sababu ya jina lake kubwa au mchango wake halisi ndani ya uwanja.
MESSI, MBAPPE NA HAALAND
Presha kwa Ronaldo iliongezeka hata kabla hajashuka dimbani. Siku moja kabla ya mechi hiyo, Lionel Messi alikuwa ameonyesha darasa la hali ya juu kwa kufunga hat-trick katika ushindi wa Argentina dhidi ya Algeria.
Mabao hayo yalimfanya kufikia rekodi ya Miroslav Klose kama wafungaji bora wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia.
Wakati huo huo, Kylian Mbappe aliiongoza Ufaransa kwa kufunga mabao mawili dhidi ya Senegal na kuweka rekodi mpya ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo.
Kana kwamba haitoshi, Erling Haaland naye alitumia mechi yake ya kwanza kabisa ya Kombe la Dunia kuonyesha kwa nini anachukuliwa kuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi duniani baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa Norway dhidi ya Iraq.
Kwa kawaida, Ronaldo amekuwa mchezaji anayependa kujibu changamoto kwa vitendo. Katika miaka yote ya ushindani wake na Messi, mara nyingi amekuwa akitumia mafanikio ya wapinzani wake kama mafuta ya kumhamasisha kufanya makubwa zaidi.
Ndiyo maana wengi walitarajia angeingia uwanjani akiwa na moto wa kuotea mbali. Lakini mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa.
URENO ILITAWALA MPIRA
Kwa kuangalia takwimu za mchezo pekee, mtu anaweza kudhani Ureno ilitawala kila kitu.
Kikosi hicho kilimiliki mpira kwa asilimia 75, kilikuwa na pasi nyingi zaidi na muda mwingi wa mchezo ulitumika katika eneo la DR Congo. Lakini soka halihukumiwi kwa umiliki wa mpira pekee.
Tatizo kubwa la Ureno lilikuwa kushindwa kubadili umiliki huo kuwa nafasi za wazi za kufunga.
Katika dakika 90, Ureno ilipiga mashuti saba, huku moja pekee likilenga lango na hilo ndilo lililozaa bao la Joao Neves mapema dakika ya sita.
Kwa timu yenye Bruno Fernandes, Bernardo Silva, Vitinha, Rafael Leao na Ronaldo mwenyewe, takwimu hizo ni za kusikitisha.
DR Congo kwa upande mwingine ilicheza kwa nidhamu kubwa, ikijilinda kwa umakini na kutumia vyema nafasi chache ilizopata.
Bao la Yoane Wissa kabla ya mapumziko liliibadilisha kabisa mechi na kuwalazimisha Wareno kuanza kucheza kwa presha.
RONALDO ALIPAMBANA NA MUDA
Katika miaka yake ya ubora, Ronaldo alikuwa tishio kila alipogusa mpira.
Alikuwa na kasi, nguvu, uwezo wa kupenya mabeki na kufunga kwa aina zote za mabao.Lakini dhidi ya DR Congo, picha ilikuwa tofauti kabisa.
Mkongwe huyo alipata miguso 25 pekee ya mpira katika dakika zote 90 alizocheza, idadi ndogo kuliko mchezaji mwingine yeyote wa Ureno aliyemaliza mechi uwanjani.
Alionekana mara nyingi akingoja huduma kutoka kwa wenzake badala ya kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mashambulizi.
Fursa zake mbili bora zaidi zilikuja katikati ya kipindi cha pili baada ya Francisco Conceicao kufanya kazi nzuri upande wa kulia.
Katika nafasi ya kwanza alichelewa kidogo kujiweka sawa na mpira ukapita pembeni ya lango.
Katika nafasi ya pili, presha ya mabeki wa DR Congo ilimfanya ashindwe kumalizia kwa utulivu na mpira ukapaa juu ya lango.
Kwa mchezaji ambaye amejenga historia yake kwa kutumia nafasi chache sana kufunga mabao, tukio hilo lilionekana kuwa ishara ya mabadiliko ya nyakati.
HILI NALO TATIZO
Mjadala mwingine ulioibuka baada ya mechi ni kama wachezaji wa Ureno wamekuwa na tabia ya kumtafuta Ronaldo kupita kiasi.
Mara kadhaa ilionekana wazi kuwa baadhi ya wachezaji walikuwa na nafasi ya kupiga mashuti wao wenyewe lakini wakachagua kutafuta pasi kwa Ronaldo.
Thierry Henry alikuwa mmoja wa waliokosoa hali hiyo.Kwa mujibu wa gwiji huyo wa Ufaransa, katika moja ya nafasi muhimu za kipindi cha pili, harakati za Ronaldo zilizuia pasi ambayo ingeweza kumfikia Bruno Fernandes katika nafasi nzuri zaidi ya kufunga.
Henry alisisitiza kuwa wakati mwingine timu inahitaji bao bila kujali nani atakayefunga.
Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa kwa sababu imegusa jambo ambalo limekuwa likizungumzwa kwa miaka kadhaa kuhusu Ureno.
Je, timu inacheza kwa ajili ya Ronaldo au Ronaldo anacheza kwa ajili ya timu?
MARTINEZ KATIKA MTIHANI MGUMU
Kocha Roberto Martinez sasa anakabiliwa na moja ya maamuzi magumu zaidi katika kazi yake.
Kwa upande mmoja anaye mchezaji ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa soka la kimataifa, nahodha wa timu na mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kutokea duniani.
Kwa upande mwingine, anayo timu yenye kizazi kipya cha vipaji ambavyo vinaonekana kuwa tayari kuchukua majukumu makubwa zaidi.
Wachambuzi wengi walishangazwa na uamuzi wake wa kutomtoa Ronaldo hata pale ilipoonekana wazi kuwa Ureno ilihitaji nguvu mpya katika safu ya ushambuliaji.
Mshambuliaji wa zamani wa England, Chris Sutton, alienda mbali zaidi kwa kusema kwamba Martinez alionekana kuogopa kumtoa Ronaldo.
Kauli hiyo imeongeza mjadala kuhusu ushawishi mkubwa wa Ronaldo ndani ya timu hiyo.
UKWELI USIOPINGIKA KUHUSU RONALDO
Pamoja na lawama zote, kuna jambo moja ambalo bado linamfanya Ronaldo kuwa muhimu.
Bado ana uwezo wa kubadilisha mechi kwa sekunde moja. Historia yake imejaa matukio ambayo alionekana kutocheza vizuri kwa dakika nyingi, lakini akafunga bao moja lililobadilisha kila kitu.
Ndiyo sababu Martinez anaendelea kumuamini. Ndiyo sababu mabeki bado wanamheshimu. Na ndiyo sababu wapinzani bado wanamwekea ulinzi maalumu.
Tatizo ni kwamba Kombe la Dunia la 2026 linaonekana kuwa na kizazi kipya cha nyota ambao wako katika kiwango cha juu zaidi kwa sasa.
Mbappe ana miaka 27 na yuko katika kilele cha uwezo wake. Haaland ana nguvu, kasi na njaa ya mafanikio. Messi, licha ya umri wake mkubwa, bado anaonekana kuwa na uwezo wa kuamua mechi kwa kiwango cha ajabu.
Ronaldo sasa anapaswa kuthibitisha kuwa bado anaweza kushindana na viwango hivyo.
DR CONGO WAMEBADILI RAMANI YA KUNDI
Wakati macho mengi yakiwa kwa Ronaldo, DR Congo wameandika historia yao wenyewe.
Pointi waliyoipata dhidi ya Ureno inaweza kuwa moja ya matokeo muhimu zaidi katika historia ya soka la taifa hilo.
Timu hiyo ilionyesha ujasiri, nidhamu na imani kubwa dhidi ya moja ya mataifa yenye vipaji vingi zaidi duniani.
Kocha Sebastien Desabre alisema siri ya mafanikio yao ilikuwa nguvu ya akili na utekelezaji sahihi wa mbinu walizopanga kabla ya mchezo.
Matokeo hayo yamebadili kabisa hesabu za kundi na kuifanya safari ya Ureno kuelekea hatua ya mtoano kuwa ngumu zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
MWISHO WA ENZI AU MWANZO WA UKOMBOZI?
Baada ya Messi, Mbappe na Haaland kuanza Kombe la Dunia kwa kishindo, Ronaldo ameanza akiwa katika hali ya kujitetea.
Hata hivyo, historia yake inaonyesha sio mchezaji wa kumchukulia poa hata kidogo. Katika maisha yake yote ya soka, amekuwa akitumia mashaka ya watu kama kichocheo cha mafanikio mapya.
Swali kubwa sasa si kama Ronaldo ni mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kutokea duniani, hilo halina ubishi.
Swali ni kama bado ana uwezo wa kuwa silaha kuu ya Ureno katika Kombe la Dunia 2026. Majibu yanaweza kupatikana katika mechi chache zijazo.