Di Maria atishiwa maisha

ROSARIO, ARGENTINA. FAMILIA ya mwanasoka, Angel Di Maria imeripotiwa kupokea vitisho vya kuuawa endapo winga huyo atarudi kwao Rosario, Argentina.

Winga huyo, 36, aliondoka kwao baada ya kuichezea mechi 36 klabu ya Rosario Central mwaka 2007 na alikwenda kujiunga na Benfica, kabla ya kutimkia Real Madrid, Manchester United, Paris Saint-Germain na Juventus.

Di Maria, ambaye aliraudi kujiunga Benfica kwenye majira ya kiangazi ameitumikia timu ya taifa ya Argentina mechi 137 na kufunga mabao 29 na alikuwamo kwenye kikosi kilichobeba Kombe la Dunia 2022 na alifunga bao kwenye mechi ya fainali.

Licha ya kuwa staa mwenye hadhi kubwa kwa nchi yake, bado familia yake imekuwa ikipokea vitisho na huko kwao Rosario, kulirushwa ndani ya nyumba kikaratasi kilichokuwa na maandishi: “Mwambie mwanao Angel asirudi Rosario tena la tutamwonyesha kwa kufanya mauaji kwenye familia yake. Hakuna atakayewasaidia hata Pullaro hataweza. Hatutarusha tena karatasi, tutarusha maiti.”

“Pullaro” ni Maximiliano Pullaro, Gavana wa Santa Fe Province.

Polisi imeanza uchunguzi juu ya wahusika wa jambo hilo ili kufahamu kwa nini mwanasoka huyo ameingia kwenye sakata hilo la kuwindwa na kundi la wahuni.a