Dembele anasakwa na Wasaudia
Muktasari:
- Sky Sports News inaeleza viongozi wakuu wa ligi hiyo tayari wameanza kufanya mawasiliano ya awali kuhusu uwezekano wa kumsajili nyota huyo wa Paris Saint-Germain.
RIYADH, SAUDI ARABIA: MATAJIRI wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia wanaandaa mikakati mikubwa dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kumsajili mshindi wa Ballon d’Or, Ousmane Dembele.
Sky Sports News inaeleza viongozi wakuu wa ligi hiyo tayari wameanza kufanya mawasiliano ya awali kuhusu uwezekano wa kumsajili nyota huyo wa Paris Saint-Germain.
Ofa kubwa sana inaandaliwa ili kujaribu kumshawishi nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa kujiunga na moja ya timu za Saudi Arabia baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia la majira ya kiangazi mwaka huu.
Mzunguko wa kwanza wa uwekezaji wa ligi hiyo katika mpango wa kusajili wachezaji wakubwa duniani unamalizika mwaka huu, huku mikataba ya nyota kadhaa wa kimataifa ikifikia tamati, hivyo mabosi wa ligi hiyo sasa wapo katika mchakato wa kutaka kusajili wachezaji wapya wenye majina makubwa.
Sky Sports News imezungumza na watu wa karibu wa fundi huyu ambao wameeleza kwa sasa Dembele hana mpango wa kuondoka badala yake nguvu amezielekezea katika kuisaidia PSG kushinda mataji kwa msimu huu pamoja na kuisaidia Ufaransa katika Kombe la Dunia.
Hata hivyo, baada ya msimu kumalizika, inaelezwa staa huyu anaweza kufikiria kuondoka na ripoti zinadai waarabu wapo tayari kumpa hadi Pauni 4000,000 kwa wiki ili akubali kujiunga nao.
Mkataba wake wa sasa umebakisha miaka miwili na nusu na PSG iko tayari kuanza naye mazungumzo kuhusu mkataba mpya, ingawa changamoto inaonekana kuwa ofa itakayompa ili asaini itakuwa ndogo kwa sababu timu hiyo kwa sasa inapambana kubana matumizi.
Mapema wiki hii rais wa PSG Nasser Al-Khelaifi alisema kila mchezaji lazima aingie katika muundo wa mishahara wa klabu.
Dembele alitangazwa mshindi wa Ballon d’Or mwaka jana baada ya kusaidia PSG kutwaa mataji matatu ikiwemo taji lao la kwanza kabisa la Ligi ya Mabingwa Ulaya.