Arteta atoa msimamo wa beki Saliba
Muktasari:
- Saliba bado ana hatihati ya kuwamo uwanjani kwenye mechi ya Jumamosi dhidi ya Wolves kwenye Ligi Kuu England, sawa na mastaa wengine kama Declan Rice, Leandro Trossard na Jurrien Timber.
LONDON, ENGLAND: KOCHA, Mikel Arteta amefunguka juu ya hali ya kiafya ya beki wa kati wa Arsenal, William Saliba.
Beki huyo wa kati wa Arsenal alipata maumivu ya enka na kukosa mechi nne za mwisho za miamba hiyo ya Emirates.
Saliba bado ana hatihati ya kuwamo uwanjani kwenye mechi ya Jumamosi dhidi ya Wolves kwenye Ligi Kuu England, sawa na mastaa wengine kama Declan Rice, Leandro Trossard na Jurrien Timber.
Alipoulizwa kuhusu Saliba, Arteta, ambaye mara zote amekuwa wakilalamika kuhusu mastaa wake kuwa majeruhi, amesema: “Ngoja tusubiri tuone. Jana hakufanya mazoezi, hajafanya mazoezi na sisi. Ngoja tuone, kama atakuwapo au la.
“Kama utaniuliza kuhusu mechi ya Everton, nadhani atakuwa fiti. Kwa mechi ya Jumamosi, sifahamu.”
Timber aliumia kwenye mechi ya kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Aston Villa na alikosa mechi ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Club Brugge kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyofanyika Jumatano iliyopita.
Alipoulizwa kuhusu Mdachi huyo, Arteta amesema: “Itategemea hali itakavyokuwa. Aligongwa na hakuwa akijisikia vizuri. Nadhani ni suala la muda. Kama atacheza mechi hii au la, ngoja tuone.”
Kiungo ghali, Rice hakusafiri na timu hiyo ilipokwenda Ubelgiji kutokana na kuwa mgonjwa na kocha Arteta alibainisha naye ni mchezaji wanayesikilizia kuhusu hali yake. Kocha huyo Mhispaniola, amekuwa na wasiwasi pia na Trossard, ambaye amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kigimbi.
MECHI ZA LIGI KUU ENGLAND WIKIENDI HII
Desemba 13, 2025
Chelsea v Everton
Liverpool v Brighton
Burnley v Fulham
Arsenal v Wolves
Desemba 14, 2025
Crystal Palace v Man City
Nottm Forest v Tottenham
Sunderland v Newcastle
West Ham v Aston Villa
Brentford v Leeds United
Desemba 15, 2025
Man United v Bournemouth