De Zerbi: Nipo tayari kushuka na Spurs
Muktasari:
- De Zerbi aliteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya Igor Tudor, akisaini mkataba wa miaka mitano huku Spurs ikiwa katika hali mbaya, pointi moja tu juu ya mstari wa kushuka daraja.
LONDON, ENGLAND: KOCHA mpya wa Tottenham Hotspur, Roberto De Zerbi amesema yuko tayari kubaki na klabu hiyo msimu ujao hata kama itashuka daraja mwishoni mwa msimu huu.
De Zerbi aliteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya Igor Tudor, akisaini mkataba wa miaka mitano huku Spurs ikiwa katika hali mbaya, pointi moja tu juu ya mstari wa kushuka daraja.
Licha ya tetesi angesubiri hadi mwisho wa msimu ndipo arejee kwenye ukocha, De Zerbi aliamua kukubali changamoto hiyo mapema, akilenga kuinusuru timu hiyo kubaki kwenye Ligi Kuu England.
“Nimeangalia mechi nyingi na ninafahamu kikosi vizuri. Hali ni ngumu, lakini ninaamini tuna uwezo wa kupambana,” amesema De Zerbi.
Kocha huyo raia wa Italia alisisitiza ana imani kubwa na ubora wa wachezaji wake, akibainisha wanachohitaji kwa sasa ni kujenga upya hali ya kujiamini.
“Tottenham ni klabu yenye historia na wachezaji wenye vipaji. Tunapaswa kukumbuka sisi ni nani na tunawakilisha nini,” aliongeza.
De Zerbi aliweka kuwa hatima ya timu hiyo haitabadilisha msimamo wake:
“Nimesaini mkataba wa miaka mitano kwa sababu naamini huu ni mradi mkubwa. Nitabaki hapa msimu ujao, bila kujali kitakachotokea.”