De Zerbi atajwa Tottenham Hotspur, wanane wakichomoza
Muktasari:
- Hatua hii imefuata baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa muda wa kikosi hicho, Igor Tudor kwa makubaliano ya pande zote mbili, baada ya kuhudumu kwa siku 44.
LONDON, ENGLAND: HAKUNA namna. Mabosi wa Tottenham Hotspur wameripotiwa kupambana kumshawishi Muitaliano Roberto De Zerbi kuchukua jukumu la kuwa kocha mpya wa kikosi hicho, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali.
Hatua hii imefuata baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa muda wa kikosi hicho, Igor Tudor kwa makubaliano ya pande zote mbili, baada ya kuhudumu kwa siku 44.
Sasa jukumu la kumpata mrithi wake limebaki mikononi mwa Mkurugenzi Mtendaji Vinai Venkatesham na Mkurugenzi wa Michezo, Johan Lange.
Inaelezwa kuwa Spurs walikuwa tayari wameamua kuachana na Tudor kufuatia kipigo cha mabao mabao 3-0 dhidi ya Nottingham Forest, matokeo yaliyoiacha timu ikiwa pointi moja tu juu ya mstari wa kushuka daraja. Hata hivyo, waliamua kumpa muda kutokana na msiba wa baba yake uliotokea hivi karibuni.
De Zerbi, ambaye kwa sasa hana timu baada ya kuondoka Marseille mapema msimu huu huku akiiongoza timu hiyo katika mechi 69, akishinda mechi 39, anaonekana kuwa chaguo la kwanza la Spurs licha ya awali kuhusishwa na Manchester United.
Kabla ya taarifa rasmi ya kuondoka kwa Tudor, klabu hiyo tayari ilikuwa imeanza kuchunguza kama kocha huyo ambaye anapendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 au 3-4-3 yuko tayari kujiunga nao.
Licha ya sasa kuwa katika hatari ya kushuka daraja, Spurs ni miongoni mwa timu kubwa nchini England ikiwa na mataji mawili ya Ligi Kuu, Kombe la FA (8), Kombe la Ligi (4) na Ngao ya Jamii (7).
Kwa upande wa Ulaya ni mabingwa wa UEFA Cup (Europa League) mara mbili na Kombe la Washindi wa Kombe la Ulaya (Cup Winners’ Cup) mara moja, pia ni wanafainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2018-19.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa De Zerbi yuko tayari kuchukua nafasi hiyo lakini angependelea iwe hadi mwisho wa msimu ili kujua kama Spurs wataendelea kubaki kwenye Ligi au la.
Akiwa na Brighton (2022–2024), aliiwezesha timu hiyo kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia kushiriki michuano ya Ulaya, ikimaliza nafasi ya sita kwenye Ligi msimu wa 2022-23, alikuwa na kiwango cha ushindi cha asilimia 52.
Kutokana na hali ya sasa ya klabu hiyo, mabosi hao wanapambana kuhakikisha kocha huyo anajiunga nao mapema iwezekanavyo ili kuinusuru kwanza na hatari ya kushuka daraja badala ya kusubiri hadi mwisho wa msimu.
Mbali na kupambana na De Zerbi, mabosi hao wanaangalia uwezekano wa kumchukua kocha Sean Dyche kwa mkataba wa muda mfupi. Dyche, ambaye aliachishwa kazi na Forest, Februari, ana historia ya kusaidia timu kuepuka kushuka daraja jambo ambalo kwa sasa ni kipaumbele kwa Spurs.
Hata hivyo, Dyche anadaiwa kuhitaji angalau mkataba wa miezi 18, hali inayoweza kuwa kikwazo katika mazungumzo yao. Kwa upande mwingine, baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wangependa kumuona akirejea Mauricio Pochettino, lakini majukumu na timu ya taifa ya Marekani kuelekea Kombe la Dunia yanafanya kuwa vigumu kupatikana kwa sasa.
Majina mengine yanayotajwa kuchukua nafasi hiyo kwa muda ni pamoja na Ryan Mason, Harry Redknapp, Tim Sherwood na Ben Davies. Pia wapo Adi Hutter, Glenn Hoddle na Chris Hughton ambao wanatajwa kama chaguo la muda.