Kompyuta imesema... Spurs haishuki daraja EPL
Muktasari:
- Tottenham huenda wataepuka kushuka daraja kwenda Championship msimu huu licha ya hofu kubwa waliyo nayo mashabiki wa kikosi hicho, kulingana na supercomputer ya Opta.
LONDON, ENGLAND: MATUMANI ya Tottenham Hotspur kusalia katika Ligi Kuu England msimu huu yapo shakani, huku kompyuta ya utabiri (supercomputer) ikitoa tathmini kuhusu hofu ya kushuka daraja kwa kikosi hicho baada ya kufungwa majuzi na Nottingham Forest.
Tottenham huenda wataepuka kushuka daraja kwenda Championship msimu huu licha ya hofu kubwa waliyo nayo mashabiki wa kikosi hicho, kulingana na supercomputer ya Opta.
Spurs walipata kipigo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Nottingham Forest, Jumapili, jambo lililoongeza wasiwasi wa timu hiyo kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu 1977 ambapo kikosi hicho cha Igor Tudor kwa sasa kipo nafasi ya 17 kikiwa na tofauti ya pointi moja tu juu ya West Ham United ilio nafasi ya 18. Ligi Kuu England ina timu 20.
Ushindi wa mwisho katika ligi kwa Spurs ulikuwa dhidi ya Crystal Palace, Desemba 28, mwaka jana takriban mechi 13 zilizopita, huku ikikusanya pointi moja tu katika mechi tano za ligi tangu Tudor achukue usukani.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Opta, Spurs ambao wamepoteza michezo sita kati ya saba iliyopita wataepuka kushuka daraja kwa tofauti ya pointi moja. Takwimu zinaonyesha West Ham United watashika nafasi ya mwisho ya kushuka daraja pamoja na Burnley na Wolverhampton Wanderers.
Mfumo huo wa Opta unawapa Spurs asilimia 27.10 ya uwezekano wa kushuka daraja ikilinganishwa na 57.48 kwa West Ham. Kwa upande wa Nottingham Forest, ushindi umeimarisha nafasi yao, huku wakipewa uwezekano wa asilimia 8.74 wa kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu 2022 chini ya kocha Vitor Pereira.
Kwingineko, Leeds United wana uwezekano wa asilimia 6.80 wa kushuka daraja, huku Crystal Palace wakiwa na uwezekano mdogo wa asilimia 0.05 chini ya kocha Oliver Glasner. Kwa mujibu wa takwimu, Wolves wana uwezekano wa asilimia 99.94 kushuka daraja wakati Burnley wako karibu sawa kwa asilimia 99.89. Katika michezo yao saba iliyobaki, Spurs watasafiri kucheza dhidi ya Sunderland, Wolves, Aston Villa na Chelsea, huku michezo ya nyumbani ikiwa dhidi ya Brighton, Leeds na Everton.
Mfumo wa Opta pia umetabiri pointi ukionyesha Wolves watamaliza mkiani wakiwa na pointi 25 wakifuatiwa na Burnley wenye pointi 26. West Ham wanatarajiwa kupata pointi 37, Spurs 38, Forest 41, Leeds 42 na Palace 48.
Akizungumza baada ya kipigo cha mwisho, kocha msaidizi wa Spurs. Bruno Saltor aliyekuwa akikaimu nafasi ya Tudor, alijaribu kubaki na matumaini licha ya hali ngumu.
“Kila kosa kwa sasa linatuathiri. Kila jambo linakwenda kinyume nasi na linaathiri pia wachezaji. Unaweza kuona (wachezaji) wanavyopambana. Tuko kwenye hali ngumu, kila mtu anajua,” alisema Saltor na kuongeza:
“Inatuumiza, inaumiza sana, lakini mashabiki wanatushangilia sana tangu kabla ya mchezo hadi mwisho. Tunapaswa kuendelea kupambana kwa sababu tunajali, tunajali Spurs, sisi ni familia na tunataka kutoka kwenye hali hii. Nina uhakika kwa asilimia 100 tunaweza kuvuka kipindi hiki.”
Spurs wana mapumziko ya wiki tatu kabla ya mechi ijayo, na Tudor atatarajia kuwa tena na wachezaji kama Mohamed Kudus na Rodrigo Bentancur baada ya kupona majeraha wakati wa mapumziko ya kimataifa.
Wakati huohuo, supercomputer pia imetabiri kuwa Arsenal watatwaa ubingwa licha ya kichapo kutoka kwa Manchester City katika fainali ya Carabao, huku Man City, Man United, Aston Villa na Liverpool wakikamilisha nafasi tano za juu kwenye msimamo.