De Jong ni kama aziita timu kijanja
Muktasari:
- Kiungo, De Jong, 27, aligomea ofa ya kwenda kujiunga na Man United kwenye dirisha la majira ya kiangazi la 2022, kipindi hicho kikosi hicho kilipokuwa chini ya kocha Erik ten Hag na mkurugenzi wa soka John Murtough, ambao walionyesha dhamira ya kuhitaji saini yake.
BARCELONA, HISPANIA: STAA wa Barcelona, Frenkie de Jong amefichua kile ambacho kitamfanya ahame kwenye timu hiyo ikiwa ni miaka miwili na nusu imepita tangu alipogoma kujiunga na Manchester United.
Kiungo, De Jong, 27, aligomea ofa ya kwenda kujiunga na Man United kwenye dirisha la majira ya kiangazi la 2022, kipindi hicho kikosi hicho kilipokuwa chini ya kocha Erik ten Hag na mkurugenzi wa soka John Murtough, ambao walionyesha dhamira ya kuhitaji saini yake.
Man United ilikubali kuilipa Barcelona ada ya Pauni 56 milioni ili kunasa saini ya kiungo huyo wa Kidachi baada ya sakata la kumsajili kuwa gumzo kwa kipindi chote cha dirisha la uhamisho la majira ya kiangazi, lakini mchezaji huyo hakushawishika kuhama Camp Nou.
Tangu wakati huo, De Jong ameshinda La Liga mara moja na Kombe la Hispania, huku akichaguliwa pia kuwa nahodha msaidizi wa timu hiyo. Kiungo huyo alikuwa panga pangua kwenye kikosi cha Xavi, lakini msimu huu ilimbidi asubiri hadi Oktoba mwaka jana kucheza mechi yake ya kwanza kutokana na kuwa na maumivu ya enka yaliyomfanya akose fainali za Euro 2024 huku Barcelona ikiwa chini ya kocha mpya, Mjerumani Hansi Flick.
Baada ya kurudi uwanjani, De Jong alishindwa kupenya kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Flick, ambapo mara yake ya mwisho kuanza ilikuwa Novemba 10. Jambo hili lilisababisha kuibuka kwa ripoti kwamba huenda kwenye dirisha hili la uhamisho wa Januari akaamua kubadili timu huku Barca ikiwa na mpango wa kutafuta pesa, hivyo nayo inaweza kushawishika kumpiga bei.
Na mwenyewe alisema: "Watu wanadhani kwamba nataka kubaki Barcelona daima kwa sababu maisha nje ya soka yapo vizuri mahali hapa, hilo ni sawa, lakini kile kinachotokea ndani ya uwanja ndicho kitu muhimu zaidi. Kama nikiona sina mchango wa kutosha, au timu ikiwa haishindani, naondoka."
Staa huyo wa zamani wa Ajax aliongeza: "Niliposaini Barcelona, sikudhani kama nitashinda tu La Liga, Copa del Rey na Spanish Super Cup baada ya miaka minne. Nilitarajia walau mara mbili ya hilo, hivyo nimehuzunika. Vitu hutokea, ambavyo huwezi kuvitabiri."
De Jong amebakiza mkataba wa miezi 18 katika klabu hiyo ya Nou Camp, hivyo Barcelona inapaswa kuangaza juu ya hatima yake mwaka huu wa 2025.