De Bruyne amkataa Drake kweupe

MANCHESTER, ENGLAND. KIUNGO wa Manchester City, Kevin De Bruyne anaweza kuwa mmoja wa watoa pasi bora zaidi Ligi Kuu England, lakini Mbelgiji huyo alilazimika kukiri kwamba hakushiriki kuandika wimbo mpya wa rapa Drake ambaye ni maarufu huko Marekani unaoitwa “Wick Man”.

Wimbo mpya wa Drake ulitolewa Ijumaa na orodha ya waliotajwa ambao walihusika nao ni kiungo huyo kama mmoja wa waandishi.

Jambo hilo limewashangaza mashabiki wakidhani kwamba mbali na kuwa mchezaji soka, De Bruyne pia  ana uwezo wa kutunga nyimbo za wanamuziki.

Kwa sasa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 anaendelea kuuguza jeraha alilopata, lakini amekanuka vikali kuhusika na wimbo huo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii.

“Drake alihitaji asisti,” De Bruyne aliandika kwa utani kwenye mitandao ya kijamii. Huo ni utani tuweke kando. Sikuhusika kabisa ila ni shabiki wake mkubwa,” aliandika De Bruyne.

Mchezaji huyo nyota anaendelea kupata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa jeraha la misuli ya paja alilopata siku ya ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu ya England Agosti, mwaka huu.

Manchester City imekosa huduma ya kiungo huyo mahiri kwa muda mrefu kutokana na jeraha hilo, ambapo mshambuliaji Erling Haaland ameandika kwenye Instagram akidai Drake siyo peke yake ambaye anahitaji pasi ya bao.

Wakati huohuo, Manchester City imepata pigo baada ya Haaland kuumia kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Faroe Island akiichezea timu yake ya taifa ya Norway na huenda akakosa mchezo unaofuata itakaokabiliana na ya Liverpool.

Mshambuliaji huyo alitokea benchi kwenye mechi hiyo ambayo Norway ilishinda kwa mabao 2-0 lakini mashabiki na kocha wa Man City, Pep Guardiola hawakupendezwa.