David Raya: Zubimendi ndiye mchezaji anayenivutia Arsenal
Muktasari:
- Arsenal waliwasajili wachezaji kadhaa waliogharimu zaidi ya Pauni 250 milioni katika dirisha la uhamisho la majira ya joto ili kuimarisha kikosi cha kocha Mikel Arteta, ambaye ana jukumu la kuipa mafanikio klabu hiyo, yenye ukame wa taji la EPL kwa zaidi ya miaka 20.
Kipa wa Arsenal, David Raya, amemchagua mchezaji aliyejiunga na klabu hiyo msimu huu wa majira ya joto ambaye amemvutia zaidi, akiwaacha wachezaji kama Viktor Gyokeres na Eberechi Eze.
Arsenal waliwasajili wachezaji kadhaa waliogharimu zaidi ya Pauni 250 milioni katika dirisha la uhamisho la majira ya joto ili kuimarisha kikosi cha kocha Mikel Arteta, ambaye ana jukumu la kuipa mafanikio klabu hiyo, yenye ukame wa taji la EPL kwa zaidi ya miaka 20.
Miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa na klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London ni Gyokeres, Eze, Martin Zubimendi, Noni Madueke, Cristhian Mosquera, Christian Norgaard, Piero Hincapie na Kepa Arrizabalaga.
Hata hivyo, Raya anaamini kuwa Zubimendi ndiye mchezaji wa Arsenal aliyetoa mchango mkubwa zaidi, tofauti na wachezaji wengine waliosajiliwa klabuni hapo msimu huu 2025-2026.
Raya ameiambia ESPN: “Nadhani ni Martin Zubimendi. Yeye ni mchezaji mjanja sana, na ameendana haraka na ligi, ambayo kuna wachezaji wengi wanaochukua muda mrefu kuzoea, hasa katika nafasi yake. Amezoea haraka sana, na unaweza kuona anachofanya kwenye timu.”
Zubimendi kutoka Hispania, alijiunga na Arsenal mwanzoni mwa msimu huu akitokea klabu ya LaLiga, Real Sociedad.
Alisajiliwa na Arteta kama sehemu ya jitihada za Arsenal kuimarisha kikosi chake, na amekuwa mchezaji muhimu kutokana na ujuzi wake wa kiufundi na uwezo wa kuzoea ligi haraka. Uhamisho huo umeipa Arsenal nguvu zaidi katikati ya uwanja na umeongeza chachu kwenye kikosi cha The Gunners.
Hadi sasa, Zubimendi amecheza mechi 14 katika mashindano yote na amefunga mabao mawili.