Daren Ferguson; Mtoto wa Sir Alex Ferguson aliyekataa historia kuandikwa

Muktasari:
- Ashley Young mwenye miaka 39 ana mtoto (Tyler Young) mwenye miaka 18 anayechezea Peterborough United F.C.
Desemba pili mwaka jana, 2024, ilifanyika droo ya raundi ya tatu (32 bora) ya Kombe la FA la England.
Katika droo hii, Everton FC ikapangwa kukutana na timu ya daraja la kwanza ya Peterborough United F.C.
Baada tu ya kutangazwa hivyo, nyota wa Everton, Ashley Young, akaandika kwenye ukurasa wa wake wa mtandao wa X, taarifa iliyobadili upepo wa mchezo huu.
WOW………. Dreams Might Come True #FaCup #GoosebumpsMoment #YoungVsYoung
Ashley Young mwenye miaka 39 ana mtoto (Tyler Young) mwenye miaka 18 anayechezea Peterborough United F.C.
Kwa hiyo mechi hii ingemkutanisha na mwanaye huyo na kuufanya mchezo huu uwe wa kwanza kumkutanisha baba na mwanaye.
Uwezekano wa baba na mwana kucheza mechi moja ukaipa mechi hii sura tofauti.
Awali mechi hii haikuwemo kwenye orodha ya mechi za kuoneshwa mbashara kwenye luninga lakini ghafla ikawekwa na muda wa mchezo kubadilishwa.
Ilipangwa kufanyika saa saba mchana Alhamisi lakini ikapelekwa saa mbili kasorobo usiku, kwa saa za England.
Saa chache kabla ya mechi Everton wakatangaza kumtimua kocha wao, Sean Dyche, na kuongeza sababu za mchezo kuzungumzwa zaidi.
Kombe la FA, mashindano makongwe zaidi katika historia ya soka duniani, yakiwa na miaka 154, yanaenda kushuhudia kwa mara ya kwanza baba na mwanaye wakikutana kwenye mechi moja.
Wakati kila mmoja akisubiri hilo, kuna mtu mmoja tu alikuwa na mipango tofauti.
Mtu huyo ni Darren Ferguson, kocha wa Peterborough United F.C ambaye ni mtoto wa kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson.
Kocha huyu ambaye anaifundisha Peterborough United F.C kwa mara ya nne, alikuwa na mawazo tofauti kabisa.
Alimuanzisha benchi Tyler Young kama ilivyokuwa kwa baba yake Ashley Young katika kikosi cha Everton.
Matarajio ya wengi Tyler ataingia...lakini aliendelea kubaki benchi hadi dakika 90 zikaisha.
BBC, TV yenye haki ya matangazo ya Kombe la FA, ilikasirika sana.
Wazee wa kuandika historia walikasirika sana na hata mashabiki wa soka wengi walikasirika sana.
Kwanini kocha hakutaka kuruhusu historia kuandikwa?
Lakini yeye mwenyewe baada ya mechi akasema yafuatayo.
“Sisi vilabu vya madaraja ya chini hatuandai vyumba vya kuvalia wachezaji kwa ajili ya timu za madaraja ya juu kuandikia historia.
Ilipotoka droo tulifurahi sana kwa sababu ilikuwa nafasi ya kwenda Goodson Park, uwanja wa kihistoria.
Mechi hii ingekuwa ya pili katika historia ya timu hizi, ya kwanza ilifanyika 2006.
Lakini zilipokuja stori za baba kucheza na mwanaye, nikaanza kuona mechi ikiharibiwa.
Vyombo vya habari havizungumzii tena kuhusu mchezo wenyewe bali baba na mtoto kucheza pamoja.
Muda wa mchezo ukabadilishwa ili kuipa nafasi luninga kuionesha mbashara.
Lakini hakuna aliyewajali mashabiki wetu ambao walitakiwa kusafiri kuja kuitazama...lakini wakashindwa.
Unaona mpira ulivyopuuzwa?
“Haya, Tyler mwenyewe hadi sasa amecheza dakika 28 tu za timu kubwa, hana uzoefu.
“Halafu mimi nimpange katika mechi kubwa kama hii ili wao wapate cha kuandika, hapana.
“Hii ni mechi kubwa na muhimu, siyo ya kirafiki au ya maonesho.
“Kombe la FA ni mashindano makubwa yanayotakiwa kuheshimiwa kwa mpira wenyewe siyo stori za baba na mwana zinazofurahisha vyombo vya habari,” alisisitiza kocha huyo.
Darren Ferguson akawa ameharibu kila kitu kwa mtazamo huu.
Ashley Young aliumia, Tyler Young aliumia, msshabiki waliumia na hata vyombo vya habari viliumia.
Lakini Darren Ferguson yeye hakujali...akaweka mbele sababu za kimpira badala za kihistoria.
Kwamba alikuwa sahihi au alikosea ni suala la mitazamo. Kila mmoja anao uhuru wa kuliangalia jambo hili kwa namna yake.
Mpira umekuwa mkubwa kama ulivyo leo siyo tu kwa sababu ya kuchezwa, bali na stori zinazouzunguka.
Vyombo vya habari vimekuwa vikikuza baadhi ya stori zinazouzunguka mpira na kuzofanya baadhi ya mechi za kawaida kuwa kubwa na kuvutia watu wengi hivyo kuifanya biashara ya mpira iwezekane na kuleta pesa ambazo yeye pia analipwa.
Kupuuza stori kama hizi haiwezi kuwa sahihi moja kwa moja.
Lakini ukija kwenye hoja za kiufundi, unaweza ukaona kocha Darren Ferguson alikuwa sahihi.
Mechi kubwa kama hizi unatakiwa kuwatumia wachezaji wako bora, na Tyler Young hakuwa mmoja wa wachezaji wake bora.
Vyovyote itakavyokuwa, mtoto wa Sir Alex Ferguson ameinyima dunia historia iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa sana.