Dani Olmo kubebwa bure kabisa
Muktasari:
- Olmo, 26, alijiunga na Barcelona, Agosti mwaka huu kwa ada ya Pauni 50 milioni akitokea RB Leipzig.
BARCELONA, HISPANIA: KIUNGO mshambuliaji wa Barcelona, Dani Olmo yupo kwenye hatari ya kuzuiwa kuitumikia timu hiyo jambo litakalomfanya aondoke bure kabisa.
Olmo, 26, alijiunga na Barcelona, Agosti mwaka huu kwa ada ya Pauni 50 milioni akitokea RB Leipzig.
Staa huyo ambaye ni zao la La Masia aliporejea Nou Camp alionekana kama usajili bora kabisa kwenye kikosi cha Barcelona kutokana na kiwango chake alichokionyesha kwenye fainali za Euro 2024, alipoisaidia Hispania kunyakua ubingwa.
Hata hivyo, Olmo ameshindwa kuandikishwa na klabu yake hiyo mpya kwa ajili ya kucheza ligi kutokana na ukata wa kifedha.
Kiungo huyo mshambuliaji alikosa mechi mbili za kwanza za Barcelona msimu huu kabla ya kuruhusiwa kucheza.
Kilichotokea ni kwamba baada ya beki Andreas Christensen kuumia na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu jambo hilo liliifanya timu hiyo inayonolewa na Hansi Flick kumwandikisha Olmo kwenye kikosi chao kama mchezaji wa dharura ili acheze.
Na katika mechi 14 alizocheza, amefunga mabao sita na asisti moja na kuisaidia timu yake kuongoza msimamo wa LaLiga. Lakini, kibali hicho cha muda cha Olmo kinamalizika mwishoni mwa mwaka huu.
Hiyo ina maana Barca inapaswa kupambana kumfanya apate nafasi ya kuorodheshwa rasmi kwenye timu. Na kama jambo hilo litashindikana, basi Olmo atakumbana na marufuku ya kuichezea klabu yake katika nusu ya pili ya msimu. Ikishindikana kabisa, basi kiungo huyo anaweza kuondoka bure.
Kiungo Olmo alifahamu mapema utata huo wakati anajiunga na Barcelona, hivyo kwenye mkataba wake uliwekwa kipengele kinachomruhusu kuondoka bure kwenye dirisha la Januari.