Dani Alves atoka gerezani

Barcelona, Hispania. Aliyewahi kuwa beki wa Barcelona ya Hispania, Dani Alves ameachiwa huru baada ya kukaa gerezani siku chache.

Alves alihukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu lakini siku chache zilizopita aliachiwa baada ya kulipa dhamana aliyotakiwa ya Pauni 850,000 zaidi ya Sh2.7 bilioni za Kitanzania.

Awali beki huyo wa zamani wa Brazil alitakiwa kutoka jana, lakini baba mzazi wa Neymar ambaye alikuwa akitajwa kuwa anakwenda kumlipia fedha hizo, hakutokea.

Pamoja na waandishi wengi kujaa nje ya gereza hilo, lakini Alves alitoka akitembea haraka akiwa ameandamana na mwanasheria wake, Ines Guardiola na kwenda kupanda gari lililoandaliwa kwa ajili yake na kuondoka eneo hilo.


Hata hivyo, Alves ni kama atakuwa kwenye kifungo cha nje, baada ya kutakiwa kuwasilisha hati zake zote za kusafiria ya Brazil na Hispania na hataruhusiwa kutoka nje ya Hispania kwa kipindi chote atakachokuwa nje.

Staa huyo aliambiwa anaweza kutoka kwenye gereza la Brians 2 lililopo karibu ya Barcelona, Jumatano iliyopita baada ya kushinda rufani yake kwamba kifungo hicho cha miaka minne anaweza kwenda kukitumikia nyumbani badala ya ndani ya gereza.

Hata hivyo, alitakiwa kulipa dhamana, ambayo aliikosa na kulazimika kubaki gerezani hadi alipotoka leo.