DAH! Ronaldo yamemkuta huko

LISBON,URENO. NYOTA wa Manchester United, Cristiano Ronaldo alijikuta ametapaa damu usoni baada ya kugongana na kipa wa timu ya Jamhuri ya Czech, Tomas Vaclik walipokua wakiwania mpira wa juu lakini kwa bahati mbaya Mreno huyo akaumia pua yake na kudondoka chini na kuzua hofu kwa wacheji wenzake.

Tukio hilo lilitokea katika dakika 12 ya mtanange huo wa michuano ya Nations League dhidi ya Czech, usiku wa kuamkia jana Ureno ikitoka na ushindi wa mabao 4-0.

Ronaldo alipatiwa huduma ya kwanza kuzuia damu iliyokuwa ikitoka na kuwekewa bandeji puani.

Baada ya ushindi huo Ureno imejikita kileleni mwa msimamo wa Group 3 la League A ya michuano hiyo ikiwa na pointi 10.

Ronaldo hakufunga bao katika ushindi huo lakini alitoa asisti kwa mchezaji mwenzake, Diogo Jota.

Staa mwenzake Ronaldo klabuni Manchester United, Bruno Fernandes alicheza soka la kiwango cha juu akifunga bao moja na kutoa asisti ya bao jingine lililofungwa na nyota mwenzao wa United, Diogo Dalot.

Kuumia kwa Ronaldo kumeamsha hofu kwa kocha wake wa United, Erik ten Hag kuelekea mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City, itakayochezwa wikiendi ijao. Hadi jana ilikuwa hakuna taarifa kamili iliyotolewa endapo Ronaldo ameumia sana kiasi cha kukosa mtanange huo.

Ushindi umeiweka Ureno kwenye nafasi nzuri ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo huku ikiwa na mechi moja mkononi.

Ureno iliwahi kubeba ndoo ya Nations League mwaka 2019 ilipoichapa Uholanzi bao 1-0 kwenye mechi ya fainali na Ureno kuandika historia mpya.