Dabi Madrid ilivyoisha na utamu, machungu
Muktasari:
- Vinicius alikuwa akikumbana na kelele za kubezwa kutoka kwa mashabiki wa Madrid mapema msimu huu baada ya kufukuzwa kwa kocha Xabi Alonso na matokeo mabaya ya aibu yaliyofuatia.
MADRID, HISPANIA: SHANGWE zilirejea kwa Vinicius Junior katika Uwanja wa Santiago Bernabeu baada ya mshambuliaji huyo wa Real Madrid kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Atletico Madrid, juzi Jumapili, na kuifanya timu yake kuendelea kuikimbiza kimyakimya Barcelona kwenye mbio za ubingwa wa La Liga.
Vinicius alikuwa akikumbana na kelele za kubezwa kutoka kwa mashabiki wa Madrid mapema msimu huu baada ya kufukuzwa kwa kocha Xabi Alonso na matokeo mabaya ya aibu yaliyofuatia.
Lakini kadri matokeo yalivyokuwa bora ndivyo mapokezi yake kutoka kwa mashabiki yalivyobadilika. Madrid imepata mafanikio makubwa chini ya kocha mpya, Alvaro Arbeloa, hasa baada ya ushindi dhidi ya Atletico kufuatia kipigo cha aibu cha mabao 5-2 Septemba 2025 pamoja na kuiondoa Man City ya Pep Guardiola katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabao mawili ya Vinicius yanaamanisha kwamba, nyota huyo wa Kibrazili amefanikiwa kuvunja rekodi yake binafsi ya kutofunga katika mechi za dabi hiyo tangu alipotua Hispania 2018-19, ikiwa na kwamba Atletico Madrid ndiyo timu ambayo amekutana nayo mara nyingi zaidi katika La Liga bila kufunga hata bao moja katika mechi 12.
Hata hivyo, kufuatia ushindi Vinicius anasifiwa kwa mchango wake mkubwa katika kurejesha kiwango cha timu, akiongoza pamoja na kiungo Federico Valverde, wakati Kylian Mbappe na Jude Bellingham wakiwa majeruhi.
Vinicius alifunga kwa penalti dakika ya 52 baada ya Ibrahima Diaz kufanyiwa faulo ndani ya eneo la hatari, huku Federico Valvede akifunga dakika ya 55 baada ya kunyang’anya mpira Jose Giminez, lakini Atletico Madrid ilipata bao la pili kupitia kwa Nahuel Molina katika dakika ya 66.
Akizungumzia kilichofanywa na Vinicius, Arbeloa alisema: “Mchezo mwingine mkubwa kutoka kwa Vini. Ameonyesha tabia na kipaji chake. Bao lake lilitupatia ushindi katika wakati mgumu. Nina bahati kuwa naye kwenye timu yangu. Bado tupo kwenye mbio za ubingwa. Kazi imekamilika.”
Katika hali ya kushangaza hayo yalikuwa mabao ya kwanza ya VinÃcius dhidi ya Atletico katika La Liga baada ya mechi 12 bila kufunga. Aliwahi kufunga mara moja tu dhidi ya timu hiyo katika mechi ya Copa del Rey na juzi alisema alipambana kuhakikisha kwamba anatimiza wajibu ipasavyo.
VinÃcius alisema: “Nimefanya kazi kwa bidii msimu mzima kwa mechi kama hizi. Sijui kwa nini, lakini kipindi hiki cha msimu kinapofika mabao na pasi za mabao huanza kuja kwa urahisi.”
Real Madrid walilazimika kujilinda dakika 12 za mwisho baada ya Valverde aliyekuwa amefunga bao kufanya 2-1 kabla ya Nahuel kusawazisha, kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea vibaya Alex Baena.
Kadi hiyo karibu iwaumize Madrid wakati Julian à lvarez alipokaribia kufunga, lakini shuti lake likagonga mwamba.
Hata hivyo, timu ya Arbeloa ilidhibiti dakika za mwisho na kuhakikisha Madrid wanaendelea kubaki nafasi ya pili, wakiwa pointi nne nyuma ya Barcelona huku mechi tisa zikiwa zimebaki.
LOOKMAN YUPO
Lookman alifikisha mabao matano tangu ajiunge na Atetico akitokea Atalanta wakati wa dirisha la usajili la Januari, baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Giuliano Simeone katika dakika ya 33. Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na gwiji wa tenisi duniani, Rafael Nadal, kutoka sehemu ya wageni maalumu uliwashuhudia wachezaji wa timu hizo mbili wakipambana kuhakikisha kila upande unaondoka uwanjani na ushindi.
Atlético wanajiandaa kwa mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona na pia fainali ya Copa del Rey dhidi ya Real Sociedad.
Jude Bellingham aliingia uwanjani dakika 15 za mwisho katika mechi yake ya kwanza tangu kuumia Februari, mwaka huu, huku Mbappe akiingia dakika ya 64 akirejea kutoka katika majeraha ya goti.
Hakuna timu iliyokuwa na kipa wake namba moja, kwani Andriy Lunin alianza kwa Madrid badala ya Thibaut Courtois, huku Juan Musso akichukua nafasi ya Jan Oblak ule wa Atlético.
Kocha wa Atletico, Diego Simeone alisema: “Tungeweza kufanya vizuri zaidi kushambulia, na tuna tumaini tutaboresha hilo katika mechi muhimu zijazo.”
TRENT NJE
Beki wa Real Madrid, Trent Alexander-Arnold, aliachwa nje ya kikosi cha kwanza katika dabi hiyo kama adhabu ya kuchelewa kuwasili.
Nyota huyo wa zamani wa Liverpool alionekana kuanza kurejea kwenye kiwango chake katika wiki za hivi karibuni, baada ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara licha ya kuanza kwa kusuasua tangu ajiunge na klabu hiyo.
Hali hiyo ilifikia kilele alipokuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Madrid dhidi ya Manchester City kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, mambo hayakwenda vizuri kwake wiki iliyoisha baada ya kuachwa kwenye kikosi cha wachezaji 35 cha timu ya taifa ya England kilichotangazwa na kocha Thomas Tuchel, jambo linaloonyesha kuwa nafasi yake ya kuingia kikosi cha mwisho cha Kombe la Dunia ni ndogo.
Na Jumapili, alijikuta tena nje ya kikosi cha kwanza Madrid, huku Dani Carvajal akichaguliwa kucheza beki wa kulia. Hatimaye aliingia uwanjani dakika 15 za mwisho kama mchezaji wa akiba. Kwa mujibu wa The Athletic, Alexander-Arnold alichelewa kufika kwenye mazoezi ya hivi karibuni, jambo lililosababisha kupoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza.