Fifa yaibania Atletico kusajili
Muktasari:
Timu hiyo ilikata rufaa yake kupinga kufungiwa kufanya uhamisho na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) hadi mwakani.
Hispania. Klabu ya Atletico Madrid imeangukia pua kutokana na rufaa yake kukataliwa na mahakama inayoshughulikia masuala ya michezo.
Timu hiyo ilikata rufaa yake kupinga kufungiwa kufanya uhamisho na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) hadi mwakani.
Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simione na wenzao Real Madrid walifungiwa kufanya usajili kwenye madirisha mawili ya usajili kutokana na kwenda kinyume na kanuni za usajili wa wachezaji wa kigeni chini ya miaka 18.
Baada ya kushindwa rufaa hiyo Fifa, Atletico waliukosa usajili wa Januari mwaka huu kutokana na kutumikia adhabu hiyo.
Hata hivyo, Atletico hawakukata tamaa na kuamua kukata rufaa ambayo imetupiliwa mbali huku wakitakiwa kuendelea kutumikia adhabu hiyo hadi msimu wa mwaka 2017-18 ili kukamilisha na dirisha la pili la usajili.
Kwa uamuzi huo, utamwathiri mchezaji wake Antonio Griezmann aliyekuwa akitakiwa na Manchester United. Pia upande wao Atletico wamezika ndoto ya kuwasajili Alexandre Lacazette kutoka Lyon, Diego Costa kutoka Chelsea.
Hivi karibuni Griezmann amekuwa kwenye joto la usajili baada ya Manchester United kupanda dali la Pauni 70 milioni, huku timu yake ikionyesha kutaka dau la Pauni 100 milioni.