Cunha: Pointi 15 ni muhimu kuliko nywele za shabiki
Muktasari:
- Endapo Man United itashinda mechi tano mfululizo Ilett atanyoa nywele zake na atazitoa kama msaada kwenda Little Princess Trust, taasisi ya inayotengeneza mawigi na kuwapa watoto waliopoteza nywele kutokana na maradhi.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa Manchester United, Matheus Cunha ametoa maoni yake kuhusu shabiki wa Manchester United ambaye ameapa kutonyoa nywele zake hadi klabu hiyo ishinde mechi tano mfululizo, akisema jamaa anawazingua na anachokifanya hakina afya kwao.
Frank Ilett, anayejulikana mitandaoni kama 'The United Strand', alitoa ahadi hiyo tangu Oktoba 2024 na hadi saasa haijatimia.
Baada ya mwanzo mzuri chini ya kocha Michael Carrick, Man United ilishinda mechi nne mfululizo ikiwamo ushindi mara mbili dhidi ya Manchester City na Arsenal, jambo lililomweka shabiki huyo karibu sana kufikia lengo lake.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, Man United ilikwama baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham United waliokuwa wakipambana kuepuka kushuka daraja.
Katika wiki iliyopita, umakini mkubwa wa vyombo vya habari ulielekezwa zaidi kwa Ilett na lengo lake la kunyoa nywele badala ya namna ambavyo Man United imejiandaa kuelekea mechi hiyo.
Akizungumza na RomarioTV, Cunha amesema wachezaji wa Man United hawaoni ahadi ya kunyoa nywele ya Ilett kuwa ni suala la kuvutia au lenye kuwahamasisha.
“Watu wanaonekana kuwa na wasiwasi zaidi kupata ushindi mara tano mfululizo kwa sababu ya nywele kuliko pointi 15. Kwa hiyo, mimi naangalia zaidi pointi 15; sijali kabisa kuhusu nywele zake.
Tunaongelea mara chache, lakini si jambo linalotuhamasisha. Hatuoni kama ni zuri. Hakuna anayetamani ushindi huo zaidi yetu na nadhani shinikizo hili la nywele zake linaficha kidogo uzuri ambao timu yetu imeonyesha walau kidogo kwa msimu huu."
Kabla ya mechi dhidi ya West Ham Jumatatu iliyopita, chanzo kimoja kiliiambia The Sun kuwa wachezaji walikuwa wanafahamu vizuri ahadi ya Ilett kuhusu nywele zake Chanzo kilisema: “Wachezaji wanafurahia sana mabadiliko chanya ya hivi karibuni na kiujumla hali kambini ni nzuri. Wanamtambua Frank kwa sababu anaonekana mara kwa mara kwenye mitandao yao ya kijamii. Baadhi yao walikuwa wanacheka na kusema: "'Haya, tumnyoe nywele huyu jamaa'."
Hata hivyo, baada ya kukosa ushindi dhidi ya West Ham, jambo hilo halikuonekana tena kuwa la kuchekesha kwao, kwani wanaona jamaa anawapa presha isiyokuwa na sababu na mada kubwa imekuwa ni wao kushinda ili yeye anyoe nywele badala ya kushinda ili timu isogee mbele zaidi.
Cunha amekuwa na msimu wa kwanza mzuri katika viunga vya Old Trafford, akifunga mabao sita ya Ligi Kuu England na akisaidia sana timu katika kupandisha mashambulizi.
Endapo Man United itashinda mechi tano mfululizo Ilett atanyoa nywele zake na atazitoa kama msaada kwenda Little Princess Trust, taasisi ya inayotengeneza mawigi na kuwapa watoto waliopoteza nywele kutokana na maradhi.