Crystal Palace yaweka rekodi Ulaya
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa Ufaransa alifunga bao la ushindi kwa shuti la karibu mwanzoni mwa kipindi cha pili mjini Leipzig, baada ya kipa kuokoa jaribio la Adam Wharton na mpira kumkuta Mateta ambaye hakukosea kuutumbukiza wavuni.
LONDON, ENGLAND: BAO la Jean-Philippe Mateta lilitosha kuipa Crystal Palace FC taji lao la kwanza kabisa la Ulaya baada ya Eagles kuifunga Rayo Vallecano katika fainali ya Europa Conference Ligi.
Mshambuliaji huyo wa Ufaransa alifunga bao la ushindi kwa shuti la karibu mwanzoni mwa kipindi cha pili mjini Leipzig, baada ya kipa kuokoa jaribio la Adam Wharton na mpira kumkuta Mateta ambaye hakukosea kuutumbukiza wavuni.
Kocha anayetarajia kuondoka Palace, Oliver Glasner, ameondoka klabuni akiwa ameiongoza kushinda ubingwa wa Kombe la FA, Ngao ya Jamii na sasa Conference Ligi katika kipindi cha kushangaza cha miaka miwili na nusu ndani ya Selhurst Park.
Timu zote mbili zilikuwa zinacheza fainali yao ya kwanza ya Ulaya, hivyo kila timu ilianza kwa tahadhari katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Red Bull haukushangaza.
Alemao alipoteza nafasi nzuri ya kufunga kwa shuti lake kutoka nje kabla ya Unai Lopez kupiga shuti lililopita pembeni mwa lango katika nafasi bora za upande wa Rayo katika kipindi cha kwanza.
Lakini nafasi kubwa zaidi ya dakika 45 za kwanza iliangukia Palace muda mfupi kabla ya mapumziko, wakati Tyrick Mitchell alipiga kichwa kilichotoka nje baada ya pasi nzuri ya Wharton ndani ya eneo la hatari.
Palace walipata bao lao dakika sita tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili wakati shuti la Wharton lilipopanguliwa na kipa wa Rayo, Augusto Batalla na kumkuta Mateta aliyefunga kwa urahisi.
Hilo lilikuwa bao la 16 la Mateta msimu huu kwa Palace, aliyekuwa karibu aondoke klabuni Januari kabla ya jeraha la goti kuzuia uhamisho wake kwenda AC Milan.
Baadaye Yeremy Pino alipiga mpira wa adhabu uliogonga mwamba mara mbili kabla ya kumtengenezea Mateta nafasi nyingine, lakini safari hii Batalla aliokoa kwa ustadi mkubwa.
Rayo Vallecano, ambao wana bajeti ndogo zaidi katika La Liga, walishindwa kutengeneza nafasi za wazi mwishoni mwa mchezo huku Palace wakidumu hadi mwisho na kuandika historia yao, pamoja na kumpa Glasner zawadi nzuri katika mchezo wake wa mwisho kama kocha wa Eagles.