Nahodha Crystal Palace apania ubingwa UEFA Conference League
Muktasari:
- Fainali hiyo dhidi ya Rayo Vallecano, itakuwa ndiyo mchezo wa mwisho kwa kocha wa Crystal Palace, Oliver Glasner, ambaye anaondoka klabuni hapo baada ya kipindi cha miaka miwili ya mafanikio makubwa kusini mwa London.
Nahodha na kipa wa Crystal Palace, Dean Henderson, amewataka wachezaji wenzake kupambana kupata ushindi wakati timu hiyo itakaposhuka dimbani kucheza mechi ya fainali ya Conference League kesho Jumatano usiku mjini Leipzig, Ujerumani.
Fainali hiyo dhidi ya Rayo Vallecano, itakuwa ndiyo mchezo wa mwisho kwa kocha wa Crystal Palace, Oliver Glasner, ambaye anaondoka klabuni hapo baada ya kipindi cha miaka miwili ya mafanikio makubwa kusini mwa London.
Glasner tayari amewafikisha ‘Eagles’ kwenye mafanikio ya kihistoria kwa kutwaa Kombe la FA na Ngao ya Jamii, na sasa anasaka zawadi ya mwisho ya kujiuzulu klabuni hapo.
Henderson aliyerithi kitambaa cha unahodha Januari 2026 kufuatia kuondoka kwa Marc Guéhi aliyetimkia Manchester City, ameeleza kuwa kikosi chao kina mshikamano mkubwa kama familia moja inayoelekea kwenye lengo moja.
Licha ya kukiri kuwa alipitia kipindi kigumu cha kushuka kisaikolojia baada ya furaha iliyopitiliza ya kutwaa Kombe la FA, kipa huyo wa England anatamani kuona kocha wao anayeondoka ambaye anamchukulia kama kocha bora zaidi kuwahi kuifundisha klabu hiyo, akiondoka kwa kishindo kikubwa cha kutwaa taji la Ulaya.
Kipa huyo alikuwa muhimili mkubwa katika ushindi wa Palace wa bao 1-0 dhidi ya Manchester City katika fainali ya Kombe la FA mwaka 2025 kwenye Uwanja wa Wembley, ambapo aliokoa penati ya Omar Marmoush na kuisaidia timu hiyo kupata taji lake kubwa la kwanza na nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu huu.
Henderson pia ameweka wazi changamoto za afya ya akili alizokutana nazo siku tatu baada ya mafanikio hayo makubwa, akidai kuwa alijisikia vibaya sana kiasi cha kutotaka hata kutoka kitandani, hali iliyomfanya ahisi kama alikuwa ameingia kwenye msongo wa mawazo ambao hajawahi kuuzungumzia popote hapo awali.
Ingawa bado haijafahamika ni nani atakayechukua mikoba ya Glasner baada ya msimu huu kukamilika, Henderson na wenzake wana nia thabiti ya kuondoka uwanjani wakiwa wameshika kombe la ubingwa.
Nahodha huyo amesisitiza kuwa timu yao haitakuwa na uoga wowote na itaingia uwanjani ikijiamini kwa hali ya juu, kwani kila mara michuano hiyo ilipokuwa migumu, wachezaji walionyesha ukomavu na kiwango bora tangu walipotoka kwenye hatua ya makundi.