Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikosi bora cha msimu Ligi Kuu England 2025-26

KIKOSI Pict

Muktasari:

  • Lakini, kwa mujibu wa mtandao maarufu wa takwimu za soka duniani wa Opta, mara baada ya msimu kumalizika umezingatia kuchagua Kikosi Bora cha Msimu wa 2025-26, ambao ulianza Ijumaa, Agosti 15, 2025 uliomalizika baada ya jumla ya mechi 380 kupigwa, mabao 1,045 kufungwa, mashuti 9,503 kufyatuliwa, pasi zilizokamilika 273,956, ‘takolingi’ 12,671 na kadi nyekundu 44.

LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England (EPL) ilimalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini kwa sasa kinachoendelea ni juu ya mambo yaliyojiri wakati mchuano wa kusaka taji hilo unaendelea, huku namba za wachezaji na michezo zikizingatiwa.

Lakini, kwa mujibu wa mtandao maarufu wa takwimu za soka duniani wa Opta, mara baada ya msimu kumalizika umezingatia kuchagua Kikosi Bora cha Msimu wa 2025-26, ambao ulianza Ijumaa, Agosti 15, 2025 uliomalizika baada ya jumla ya mechi 380 kupigwa, mabao 1,045 kufungwa, mashuti 9,503 kufyatuliwa, pasi zilizokamilika 273,956, ‘takolingi’ 12,671 na kadi nyekundu 44.

Mwisho wake ulishuhudia Arsenal ikitwaa ubingwa huku West Ham United, Burnley na Wolverhampton Wanderers zikishuka daraja. Huu ni uchambuzi wa kiwango cha kila mchezaji uliolenga kuchagua cha Opta, ambapo mastaa 11 wamechaguliwa baada ya kufanya vizuri zaidi ya wengine katika nafasi zao kulingana na takwimu.

KIKO 02

KIPA

David Raya (Arsenal); huyu ni kipa wa mabingwa anayeingia katika kikosi bora baada ya kufanya sevu muhimu zilizoisaidia Arsenal kumaliza ukame wa miaka 22 bila ubingwa wa ligi.

Mhispania huyo alitwaa tuzo ya Kipa Bora (Golden Glove) kwa msimu wa tatu mfululizo akimaliza akiwa na clean sheet 19, nyingi zaidi kwa ligi nzima. Idadi hiyo ilisawazisha rekodi ya klabu katika msimu mmoja iliyowahi kuwekwa na David Seaman misimu ya 1993-94 na 1998-99.

Raya alianza mechi nyingi zaidi (37) na kucheza dakika nyingi zaidi (3,300) kuliko mchezaji mwingine yeyote wa Arsenal katika msimu huu wa ubingwa, akikosa mchezo wa mwisho pekee dhidi ya Crystal Palace baada ya ubingwa kuwa tayari umehakikishwa.

KIKO 01

BEKI WA KULIA

Matheus Nunes (Manchester City); kwa mchezaji aliyekuwa akionekana kufaa zaidi kiungo ameonyesha kiwango bora tangu abadili nafasi na kucheza upande wa kulia wa safu ya ulinzi ya Manchester City.

Takribani asilimia 98 ya dakika zake zote EPL msimu huu alicheza kama beki wa kulia. Ubora wake akiwa na mpira ulimfanya kuwa moja ya silaha muhimu za City. Kati ya mabeki wa pembeni, Nunes alikuwa alikokota mipira mara nyingi zaidi (514) na alikimbia umbali mrefu zaidi akiwa na mpira (mita 5,575). Pia alikamilisha pasi 1,153 katika nusu ya wapinzani zikiwa ni nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote ligi nzima na kwa usahihi wa asilimia 88.4. Katika ulinzi pia alikuwa mgumu kupitwa. Asilimia yake ya ushindi katika ‘takolingi’ ilikuwa asilimia 67, ya pili kwa ubora ndani ya Manchester City nyuma ya Ruben Dias aliyekuwa na asilimia 72.2.


MABEKI WA KATI

William Saliba (Arsenal); akiwa sehemu ya ukuta imara wa Arsenal, William Saliba aliunganisha nguvu na Gabriel Magalhaes kwa utulivu na umaridadi. Mfaransa huyo alipitwa kwa chenga mara saba tu katika EPL msimu huu, akiwa miongoni mwa mabeki waliocheza dakika nyingi kama zake Virgil van Dijk (mara mbili) na Ezri Konsa (mara nne) pekee waliopitwa mara chache zaidi. Saliba pia alikuwa bora akiwa na mpira akikamilisha asilimia 92.9 ya pasi zake kikiwa ni kiwango cha tatu bora kwa wachezaji waliopiga pasi zaidi ya 2,000 msimu huu. Pamoja na Gabriel, waliunda safu bora zaidi ya ulinzi ligi nzima, Arsenal wakitunza clean sheet 15 katika mechi 26 walizoanza pamoja.

Gabriel Magalhaes (Arsenal)

Gabriel alikuwa moja ya nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya Arsenal iliyotwaa ubingwa, akimaliza akiwa na clean sheet 17 zikiwa ni nyingi zaidi kwa beki yeyote katika ligi hiyo huku Arsenal wakiruhusu mabao 27 pekee msimu mzima. Akiwa uwanjani, Arsenal waliruhusu mabao 20 ukiwa ni wastani bora zaidi kwa mabeki waliocheza zaidi ya dakika 2,000. Mbali na ulinzi, Gabriel aliendelea kuwa tishio kubwa katika mashambulizi ya mipira ya adhabu, akifunga mabao matatu na kutoa asisti nne, huku akiwa mchezaji aliyegusa mpira kwanza mara nyingi zaidi katika kona za Arsenal (13).


BEKI WA KUSHOTO

Adrien Truffert (Bournemouth); aliyesajiliwa kutoka Rennes msimu uliopita, Adrien Truffert aliwasili Bournemouth akiwa na jukumu kubwa kuziba nafasi ya Milos Kerkez. Truffert aling’ara katika msimu wake wa kwanza, akiwa mchezaji pekee kufanya mikimbio mingi ya kuwapita wapinzani (overlapping runs) zaidi ya 50 katika Ligi Kuu England 2025-26. Pia alitoa asisti tano, huku Lucas Digne pekee akiwa na asisti nyingi zaidi miongoni mwa mabeki na katika ulinzi, Truffert alikuwa na ‘takolingi’ nyingi zaidi (103) na kuingilia pasi (interceptions) nyingi zaidi (48) kuliko beki mwingine yeyote wa pembeni. Pia alikuwa mchezaji pekee wa Bournemouth kuanza mechi zote 38 za ligi.

KIKO 03

VIUNGO WA KATI

Dominik Szoboszlai (Liverpool); licha ya Liverpool kumaliza nafasi ya tano, Dominik Szoboszlai alikuwa bora binafsi akifunga mabao manne kutoka nje ya eneo la hatari yakiwa ni mengi zaidi sambamba na wengine, huku yote yakitokana na mipigo huru ya adhabu (free-kick) za moja kwa moja. Pia alikuwa tishio kubwa katika ubunifu akitengeneza nafasi nyingi kutokana mipira ya adhabu na kupiga krosi zilizofanikiwa nyingi zaidi (69).

Declan Rice (Arsenal); huyu anaingia katika Kikosi Bora cha Premier League kwa msimu wa nne mfululizo, safari hii akiwa bingwa wa ligi. Hakuna mchezaji wa Arsenal aliyecheza dakika nyingi zaidi kuliko Rice (3,099), alitengeneza nafasi 63 kwa wenzake huku akiwa mmoja wa wabunifu wakubwa wa timu. Kutoka katika kona na mipigo huru ya adhabu (free-kick) isiyo ya moja kwa moja, Rice alikuwa na mara tatu kwa  kiwango cha juu zaidi ligi nzima. Katika upande wa ulinzi, aliongoza Arsenal kwa kurejesha umiliki mipira (possession regains) kwa dakika 90.

Elliot Anderson (Nottingham Forest); mwamba huyu alikuwa na msimu bora akiwa Nottingham Forest na ndiye mchezaji pekee katika kikosi  kutoka timu iliyomaliza nusu ya chini ya msimamo. Alikuwa na miguso (touches) nyingi zaidi (3,300), alishinda mipambano ya kugombea mpira (duels) mingi zaidi (298), alipora mipira mingi zaidi (306) na alichezewa faulo nyingi zaidi (80) kuliko mchezaji mwingine yeyote EPL. Pia alikamilisha pasi nyingi zaidi (2,038) na pasi zinazopenya au kuvunja mistari ya ulinzi au kiungo cha wapinzani (line-breaking passes) nyingi zaidi (376) miongoni mwa viungo wa kati.

KIKO 04

VIUNGO WASHAMBULIAJI

Bruno Fernandes (Manchester United); nyota huyu alivunja rekodi ya asisti nyingi zaidi katika msimu mmoja wa EPL akiwa nazo 21, akiipiku rekodi ya asisti 20 iliyowahi kuwekwa na Thierry Henry na Kevin De Bruyne. Nahodha huyo wa Man United pia alitengeneza nafasi 136 kwa wachezaji wenzake zikiwa ni nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote. Alimaliza msimu akiwa amehusika katika mabao 30 (akifunga tisa na asisti 21). Rayan Cherki (Manchester City); huyu alikuwa na msimu bora katika mwaka wake wa kwanza Manchester City akitoa asisti 12, idadi kubwa zaidi kwa mchezaji anayecheza mara ya kwanza katika ligi tangu Dimitri Payet 2015-16. Ni Bruno pekee aliyekuwa akitengeneza nafasi nyingi zaidi kwa dakika 90 kuliko Cherki.

KIKO 05

STRAIKA

Erling Haaland (Manchester City); mwamba kabisa aliyetwaa tena Kiatu cha Ufungaji Bora EPL (Golden Boot) baada ya kufunga mabao 27.

Ameingia katika orodha ya wachezaji watano pekee kushinda tuzo hiyo mara tatu au zaidi akiwa pamoja na Thierry Henry, Mohamed Salah, Alan Shearer na Harry Kane. Msimu huu pia alitoa asisti nane na kuendelea kuwa na kiwango bora cha kutumia nafasi zake, akifunga kwa asilimia 21.4 ya mashuti yake yote.