Cole Palmer nje wiki mbili
Muktasari:
- Palmer mwenye umri wa miaka 23, amekuwa akikabiliana na tatizo la nyonga (groin) tangu mwanzo wa msimu huu na kila siku hali yake imezidi kuwa siyo nzuri.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amethibitisha staa wa timu hiyo, Cole Palmer atakuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili hadi tatu.
Palmer mwenye umri wa miaka 23, amekuwa akikabiliana na tatizo la nyonga (groin) tangu mwanzo wa msimu huu na kila siku hali yake imezidi kuwa siyo nzuri.
Nyota huyo alicheza mechi kwa dakika 90 mara moja tu katika ligi msimu huu kutokana na maumivu hayo na ilisababisha atolewe uwanjani dakika ya 18 katika mechi dhidi ya Manchester United.
Maresca amefichua ameamua kumpumzisha staa huyo ili kumruhusu apone kabisa badala ya kuhatarisha afya yake kwa kuendelea kumchezesha.
"Tumeamua kumlinda kidogo Cole ili jeraha lake lisizidi kuwa baya. Tumeamua kumpumzisha kwa wiki mbili hadi tatu zijazo kabla ya mapumziko ya kimataifa kuona kama anaweza kupona kwa asilimia 100 na kurudi akiwa fiti baada ya mapumziko hayo."
Kuumia kwa Palmer linakuwa ni pigo kubwa kwa Chelsea kwani atakosa mechi za Ligi Kuu England dhidi ya Brighton na Liverpool, pamoja na mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica.
Vilevile litaendelea kuwa pigo kwa kocha wa England, Thomas Tuchel, kwani anaweza kumkosa staa huyo katika mechi dhidi ya Wales na Latvia mwezi ujao.
Jeraha hili la nyonga tayari lilimfanya akose kambi ya timu ya taifa ya England Septemba na akakosa mechi dhidi ya Andorra na Serbia mapema mwezi huu.
Kwa bahati nzuri, jeraha hilo halionekani kuwa la muda mrefu kwani Maresca amethibitisha hatofanyiwa upasuaji.
"Sidhani kama anahitaji upasuaji. Ni suala tu la kumpumzisha kutokana na maumivu yake ya nyonga."
Mbali ya Palmer, Tosin Adarabioyo naye amepata jeraha jipya litakalomweka nje hadi baada ya mapumziko ya kimataifa.
Chelsea tayari inawakosa wachezaji wengine wakubwa kama Levi Colwill na Liam Delap kutokana na majeraha waliyopata mwanzoni mwa msimu huu.