Jeraha la Palmer tatizo Chelsea
Muktasari:
- Palmer alianza mechi ya kwanza ya Chelsea ya Ligi Kuu England msimu huu dhidi ya Crystal Palace lakini alikosa michezo iliyofuatia dhidi ya West Ham United na Fulham.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA ipo katika njia panda kuhusu mbinu gani katika kutibu tatizo la nyonga la staa wao Cole Palmer, ambaye kuna njia nyingi ikiwamo upasuaji.
Palmer alianza mechi ya kwanza ya Chelsea ya Ligi Kuu England msimu huu dhidi ya Crystal Palace lakini alikosa michezo iliyofuatia dhidi ya West Ham United na Fulham.
Alionekekana uwanjani akitokea benchini katika mechi dhidi ya Brentford na akaanza tena kwenye kikosi cha kwanza katika mechi ya ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, akifunga mabao kwenye michezo yote hiyo miwili.
Palmer alianza tena mechi dhidi ya Manchester United Jumamosi iliyopita, lakini alilazimika kutoka baada ya dakika 20 tu katika kipindi cha kwanza.
Chelsea imekuwa ikijaribu kudhibiti tatizo la nyonga ambalo Palmer aliingia nalo kwenye msimu huu, lakini kitendo cha kulazimika kutoka mapema dhidi ya Man United kimezua hofu kubwa.
Palmer hakucheza katika mechi ya Carabao Cup dhidi ya Lincoln City Jumanne, ambapo baada ya mechi kocha Enzo Maresca alifichua wiki hii kuwa kutakuwa na kikao cha kuamua njia bora ya kumsaidia kupona kabisa tatizo.
Maresca amekuwa akisema mara kadhaa msimu huu kwamba Palmer “anapimwa kila siku”, kujua hali yake kabla ya kumruhusu kucheza mechi yoyote jambo ambalo sasa halionekani kuwa na afya kwani hali yake inazidi kuwa mbaya.
Chelsea inapanga kutumia njia kadhaa ili kumsaidia kupona, kwanza ni kumpumzisha kwa muda wa hadi wiki nne. Stephen Smith, Afisa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Kitman Labs (kampuni inayojikita kwenye uangalizi wa majeraha), amesema hilo sasa linaweza kuwa chaguo.
Vilevile upasuaji pia ni njia nyingine lakini haishauriwi sana kwa sasa.
"Ni vigumu sana kusema wiki zijazo zitakuwaje. Chelsea wanaangalia namna ya kufanya. Moja ni kuendelea kudhibiti tatizo lake kwa kumtibia huku akiendelea kutumika au wamuache apumzike kwa muda usiopungua wiki nne hali ambayo itamfanya kupata afadhali na mwisho wanafikiria kumfanyia upasuaji ambao utamponya kabisa."