Chido Obi amtumia meseji kocha Amorim
Muktasari:
- Aliingizwa kwenye dakika tatu za mwisho kuchukua nafasi ya kiungo Casemiro wakati huo Man United ikiwa nyuma kwa bao 1-0. Hakuna na muda wa kutosha kuleta madhara na hivyo timu yake ikapoteza mechi.
MANCHESTER, ENGLAND: STRAIKA kinda wa Manchester United, Chido Obi amemtumia ujumbe kocha wa timu hiyo Ruben Amorim baada ya kumpa muda mchache wa kucheza mechi yake ya Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham, Jumapili.
Chido, 17, alicheza kwenye kikosi cha kwanza katika mechi hiyo ya ligi iliyopigwa uwanjani Tottenham Hotspur.
Aliingizwa kwenye dakika tatu za mwisho kuchukua nafasi ya kiungo Casemiro wakati huo Man United ikiwa nyuma kwa bao 1-0. Hakuna na muda wa kutosha kuleta madhara na hivyo timu yake ikapoteza mechi.
Licha ya kipigo hicho, Obi alimshukuru Amorim kwa kumpa nafasi ya kwanza kucheza kwenye kikosi cha wakubwa, alisema: "Nimehuzunika kupoteza. Kwa upande wangu binafsi, namshukuru kocha kwa kutimiza ndoto zangu pamoja na familia yangu."
Mashabiki walivamia ukurasa huo wa Chido na kutoa meseji zao na wa kwanza alisema: "Mwanzo wa jambo kubwa." Mwingine alisema: "Muda wako umewadia."
Shabiki wa tatu alisema: "Hongera. Nafasi nyingi zaidi zitakuja."
Kuna mashabiki wamemshambulia kocha Amorim alikuwa mwoga kwa kushindwa kumwingiza Obi mapema katika mechi hiyo na kusubiri dakika tatu za majeruhi.