Chelsea yashusha Presha

Wednesday April 07 2021
chelsea pc
By Juma Mtanda

KUELEKEA mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya FC Porto, Chelsea imezidi kuongeza matumaini baada ya nyota wake N'Golo Kante na Christian Pulisic kurejea kwenye kikosi wakiwa wamepona majeraha.

Taarifa za wachezaji hao kuwa sawa kwa ajili ya mechi hiyo zimethibitishwa na kocha wao, Thomas Tuchel ambaye amesisitiza watasafiri na timu.

Kante aliukosa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya West Brom ambapo Chelsea ilibamizwa mabao 5-2 kwa sababu alikuwa na maumivu ya misuli wakati Pulisic alitolewa nje baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kutokana na maumivu ya nyama za nyuma ya paja.

Mchezaji mwingine aliyerejea kutoka kwenye majeraha na anaweza kucheza mechi hiyo ni  Tammy Abraham aliyekosekana kwenye mechi nane kutokana na majeraha ya mguu.

"Wapo sawa na watakuwa kwenye kikosi, kwahiyo hii ni habari nzuri.Christian  alikuwa kwenye kiwango kizuri kabla hajapata majeraha, kwenye mchezo uliopita aliniambia  anahisi maumivu hivyo alihofia ikiwa ataendelea kucheza huenda angejisababishia majeraha makubwa zaidi ambayo yangemfanya kukaa nje kwa muda mrefu "alisema Tuchel na kuongeza,

"Tammy atakuwa kwenye kikosi  na Kante naye pia ni hivyo hivyo ingawa ataanzia benchi,"

Advertisement

Mechi hii ya  Chelsea inatarajiwa kupigwa saa 4:00 usiku, lakini mbali ya hii kutakuwa na mtanange mwingine kati ya Bayern Munich  itakayokuwa nyumbani ikiikaribisha PSG.  

Advertisement