Chelsea yashika pointi za ubingwa, Top Four unyama mwingi

LONDON, ENGLAND. CHELSEA imeshika pointi tatu za kuamua bingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Bila shaka, Arsenal wataweka uhasama wao wa London pembeni na kuomba The Blues wakaze hiyo kesho Jumapili kufanya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England ziendelee kuwa hai walau kwa wiki moja zaidi.

Lakini, swali linaloulizwa, Chelsea hiyo ya Frank Lampard itaweza kuzuia moto ule wa Manchester City kwa sasa?
Mbaya zaidi, kipute hicho kitapigwa Etihad. Chelsea watakomaa wasigawe pointi tatu kwa Man City? Kilichopo ni kwamba Man City wanahitaji pointi tatu tu kubeba taji lao la tatu mfululizo la Ligi Kuu England na taji la tano katika misimu sita ya mwisho.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amewaambia mastaa wake wamalizane na ishu ya ubingwa wa Ligi Kuu England mapema ili wafikirie mataji mengine waliyobakiza msimu huu. Kitu kibaya kwa Chelsea katika kuwazuia Man City katika mechi hiyo ni kwamba Guardiola na chama lake huu ni mchezo wao wa mwisho wa ligi uwanjani Etihad, hivyo watataka kumaliza shughuli mapema mbele ya mashabiki wao.

Rekodi zinaonyesha kwamba Man City na Chelsea zimekutana mara 51 kwenye Ligi Kuu England, huku The Blues ikishinda 27, mara 14 nyumbani na 13 ugenini. Hiyo inaonyesha kwamba Chelsea si wanyonge wanapokuwa ugenini kuwakabili Man City, ambao wenyewe wameshinda mara 17, mara 10 nyumbani na saba ugenini. Mechi saba baina yao zilimalizika kwa sare. Lakini, mechi tano zilizopita walipokutana, Man City imeshinda nne, ikiwamo tatu za mwisho na Chelsea wamepata ushindi mara moja tu. Je, watagoma kutoa ubingwa, au watatoa? Kazi kwa Lampard na Chelsea.

Hata hivyo, Arsenal ambao wanaombea Chelsea waikazie Man City hiyo kesho ili wasitangaze ubingwa, shughuli yao wao ni leo, Jumamosi watakapokuwa huko City Ground kukipiga na Nottingham Forest. Kocha Mikel Arteta na Arsenal yake watahitaji kushinda mechi ili dua zao ziendelee kuwa salama, la wakichapwa basi Man City haitahitaji ushindi wowote mbele ya Chelsea watakuwa wameshatangaza ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Kwa hiyo, Arsenal wajibebe wenyewe kwanza kabla ya kuomba kubebwa na Chelsea. Rekodi zinaonyesha Arsenal haipo vibaya kwenye mechi 11 ilizocheza na Forest kwenye Ligi Kuu England imeshinda saba, nne nyumbani na tatu ugenini, huku Forest wakishinda moja tu, ambayo walicheza nyumbani. Mechi tatu zilimalizika kwa sare. Mechi ya mzunguko wa kwanza kwenye ligi msimu huu, Arsenal iliichapa Forest 5-0, huku mara ta mwisho Forest kuichapa Arsenal uwanjani City Groud ilikuwa Desemba 1996.

Kipute cha mapema kabisa leo Jumamosi kitakuwa huko London, wakati Tottenham Hotspur itakapojaribu kusaka tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao kwa kuwakabili Brentford, ambao nao wanataka kucheza Ulaya msimu ujao. Spurs na Brentford zimekutana mara tatu kwenye Ligi Kuu England, ambapo mechi mbili zilimalizika kwa sare, huku Spurs ikishinda moja ilipocheza nyumbani. Mechi zao mbili za mwisho walipokutana, zilimalizika kwa sare. Safari hii itakuwaje?

Manchester United baada ya kupewa presha kubwa na Newcastle United kwenye mbio ya Top Four, watakuwa ugenini kukipiga na Bournemouth. Newcastle waliichapa Brighton usiku wa juzi Alhamisi na hivyo kuweka pengo la pointi tatu dhidi ya Man United kwenye nafasi ya tatu na nne, lakini wakiwa na mechi moja zaidi, hivyo Man United watahitaji ushindi wa ugenini uwanjani Vitality ili kuwafikia kwa pointi Newcastle, lakini pia wakiwakimbia Liverpool, ambao wanaonekana kukoleza moto kwenye kuisaka Top Four.

Man United na Bournemouth zimekutana mara 11 kwenye Ligi Kuu England, ambapo Mashetani Wekundu wameshinda nane, tano nyumbani na tatu ugenini, huku Bournemouth wakishinda mbili tu, zote nyumbani na kuna mechi moja ilimalizika kwa sare. Mechi tano za mwisho walizokutana, Man United imeshinda nne, Bournemouth moja.

Liverpool wanaoisaka Top Four kwa udi na uvumba, watakuwa nyumbani Anfield kuwakabili Aston Villa, ambao wamekuwa moto kwelikweli tangu walipoanza kunolewa na Mhispaniola, Unai Emery. Jurgen Klopp na kikosi chake cha Liverpool kimeachwa pointi moja tu nyuma ya kutinga Top Four, hivyo watahitaji kushinda mechi yao na mengine wataacha yajitengeneze yenyewe. Rekodi zinaonyesha, Liverpool na Aston Villa zimekutana mara 55 kwenye Ligi Kuu England, huku Liverpool ikishinda 32, mara 16 nyumbani na 16 ugenini, wakati Aston Villa imeshinda 13 tu, saba nyumbani na sita ugenini, pia kukiwa na mechi 10 zilizomalizika kwa sare. Mechi tano zilizopita, Liverpool wameichapa Aston Villa mara nne na kupoteza moja tu, wakati walipochapwa 7-2, Oktoba 2020.

Mechi nyingine Fulham itakipiga na Crystal Palace huko Craven Cottage. Miamba hiyo imekutana mara tisa kwenye Ligi Kuu England, sare mbili, Fulham imeshinda tatu, moja nyumbani na mbili ugenini, huku Palace ikishinda nne, mbili nyumbani na mbili ugenini.

Shughuli pevu nyingine itakuwa huko Molineux, wakati Wolves itakapokabiliana na Everton, mechi iliyobeba vita ya kujiondoa kwenye sakata la kushuka daraja. Wolves hawana shida, ila wasiwasi wa kushuka upo kwa Everton jambo litakalofanya mechi kuwa tamu zaidi. Miamba hiyo imekutana mara 17 kwenye Ligi Kuu England, huku kila timu ikishinda mara sita na mechi tano zilizimaliza kwa sare. Wolves mechi zake sita ilizoshinda, tatu zilikuwa nyumbani na tatu ugenini, huku Everton wao ushindi wao mara sita, nne walipokuwa nyumbani Goodison Park na mbili ugenini.

Shughuli ya kesho, ukiacha kipute cha kutangaza ubingwa huko Etihad, kutakuwa na mechi mbili nyingine, ambapo West Ham United watakuwa nyumbani kukipiga na Leeds United, wanaotafuta pointi za kuwaondoa kwenye kasheshe la kushuka daraja. West Ham na Leeds zimekutana mara 25 kwenye Ligi Kuu England, ambapo kwenye mechi hizo, tano zilimalizika kwa sare, Leeds inishinda 15, nane nyumbani na saba ugenini na West Ham imeshinda tano tu, mbili nyumbani na tatu ugenini. Walipokutana msimu huu, walitoka sare ya mabao 2-2 uwanjani Elland Road. Leeds watachomoka? Ngoja tuone.

Brighton baada ya kuchapwa na Newcastle watakuwa na kazi mbele ya Southampton, ambayo tayari imeshashuka daraja msimu huu. Miamba hiyo imekutana mara 11 kwenye Ligi Kuu England, na sita zilimalizika kwa sare, huku Brighton ikishinda mbili, zote ugenini na Southampton imeshinda tatu, nazo pia ugenini. Upekee wa timu hizo zilipokutana, hakuna iliyoshinda nyumbani. Keshokutwa Jumatatu, kutakuwa na mechi moja tu, Newcastle watakuwa St James' Park kukipiga na Leicester City, wanaopambana pia wasishuke daraja. Newcastle wanataka tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na hicho ndicho kinachofanya mechi hiyo kuwa na mvuto wa kipekee.

Zimekutana mara 31 kwenye Ligi Kuu England, Newcastle ikishinda 14, nane nyumbani na sita ugenini, huku Leicester City ikishinda 12, sita nyumbani na sita ugenini, wakati kuna mechi tano zilimalizika kwa sare. Mechi tano zilizopita walipokutana, Newcastle imeshinda tatu na Leicester mbili.