Chelsea yaibiwa kamera mazoezini
Muktasari:
- Chelsea imekuwa ikifanya mazoezi huko Cobham, Surrey tangu 2005 kabla ya kituo hicho kufunguliwa rasmi miaka miwili baadaye.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imeripotiwa kupiga simu polisi kuripoti tukio la kupotea kwa kamera yenye thamani ya Pauni 30,000 kwenye uwanja wake wa mazoezi.
Chelsea imekuwa ikifanya mazoezi huko Cobham, Surrey tangu 2005 kabla ya kituo hicho kufunguliwa rasmi miaka miwili baadaye.
Wachezaji wa kikosi cha kwanza walirejea mazoezini Cobham mapema wiki iliyoisha kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu England utakaoznaa mwishoni kwa wikiendi ijayo. Lakini, baada ya kuona kamera ya thamani ya Pauni 30,000 haipo kwenye viwanja hivyo, imetoa taarifa kwenye kituo cha polisi cha Surrey.
Ilidhaniwa kwamba kifaa hicho kitakuwa kimewekwa sehemu na kwamba kitaonekana baada ya maofisa wahusika kurejea baada ya mapumziko.
Hata hivyo, Chelsea imeamua kupiga simu polisi kuripoti suala hilo.
Kama ilivyo kwa klabu nyingi kubwa za soka, Chelsea imekuwa ikitumia teknolojia ya kamera kwa ajili ya mazoezi na masuala ya mitandao ya kijamii.
Picha za video zinazonaswa kwenye viwanja vya mazoezi na mechi zinasaidia wachezaji kutambua vitu kadhaa vya kiufundi, fiziki na mbinu sambamba na kuboresha ubora wa viwango vya kiakili.
Viwanja hivyo vya mazoezi ya Chelsea zimeripotiwa kugharimu Pauni 20 milioni na vipo umbali usiozidi maili 20 kusini magharibi mwa Stamford Bridge.
Wachezaji kama Raheem Sterling na Reece James waliwahi kuvamiwa na wezi kwenye makazi yao ambayo yapo karibu na eneo hilo la viwanja vya mazoezi ya Chelsea. Vidani na saa za thamani ziliibwa nyumbani kwa Sterling wakati alipokuwa akiitumikia England katika fainali za Kombe la Dunia 2022.
Nahodha wa Chelsea, James nyumba yake ilivamiwa na wezi wakati akiwa kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021.
Chelsea ilitarajia kurudi Stamford Bridge wikiendi hii kwa kucheza mechi mbili za kirafiki za pre-season dhidi ya Bayer Leverkusen iliyopangwa kufanyika jana Ijumaa na itakipiga na AC Milan, Jumapili.
Chelsea itaanza msimu wa Ligi Kuu England 2025/26, Agosti 17 kwa kukipiga na mabingwa wa Kombe la FA, Crystal Palace. Kisha itacheza na West Ham, Fulham na Brentford kabla ya kuifuata Manchester United katika mechi tano za kwanza.